Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 06, 2022 Local time: 10:38

Tanzania : Waziri Simbachawene asema Mchungaji Mwamposa atawajibishwa


Waziri Simbachawene

Watu 20 wamekufa Jumamosi Februari 1, 2020 kutokana vurugu za waumini kukanyangana katika harakati za kujaribu kufikia mafuta ya upako kwenye kongamano la mahubiri ya Mchungaji Boniface Mwamposa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene amesema kiongozi huyo wa kidini anatakiwa kuwajibika kwani hakuchukuwa tahadhari wakati wa kuwakusanya waumini katika ibada hiyo na hivyo serikali lazima ichukue hatua zinazostahiki.

“Kwa sababu inasikitisha kuna idadi kubwa ya watu umewakusanya mahala, mwenye jukumu la kuhakikisha usalama wao ni wewe uliyewakusanya hapo, pamoja na jukumu la serikali kuhakikisha watu wako salama. Kwa idadi kubwa ya watu kama hiyo unapotoa maelezo au maneno ambayo yanaweza kusababisha mhemko na watu wakaweza kukimbizana na kufikia hatua ya kuumia basi una wajibu wa kuwajibishwa katika kosa hilo.

“Kwa hiyo nitoe rai kwa viongozi wa madhehebu na shughuli za kidini na mikusanyiko mbalimbali kujua kwamba wanao wajibu wa kuhakikisha usalama wa watu hao. Mchungaji au mtume Boniface Mwamposa baada ya tukio hili alitaka kukimbia. Lakini hivi ninavyo zungumza yuko katika mikono ya Jeshi la polisi. Na tunafikiria kumtoa Dar es Salaam kumrudisha Moshi ili aende akawajibike kwa kosa au madhara haya ya maafa ambayo kwa kweli kwa uwazi yeye na wenzake wamesababisha,” ameeleza waziri.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba alithibitisha taarifa hizo za awali juu ya waumini 20 kufa.

“Taarifa za awali tulizonazo ni kuwa ni waumini 20 wamepoteza maisha lakini tunaendelea kufuatilia maeneo mengine ya zahanati, vituo vya afya na hospitali kama kuna watu walipelekwa huko,” amesema Kippi.

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa waumini hao walikumbwa na maafa hayo wakati wakikanyagana kwa ajili ya kugombania kukanyaga mafuta yaliyomwagwa na mhubiri huyo yakidaiwa kuwa na upako.

Inaelezwa kuwa watu zaidi ya 40 walikanyagana katika harakati za kugombania mafuta ya upako na kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

Idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka kwa kuwa hakuna taarifa ya ujumla ya majeruhi waliopelekwa katika vituo vya afya vya jirani pamoja na Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG