Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 22:58

Mkuu wa Mkoa Makonda ataka Tundu Lissu asijadiliwe


Tundu Lissu
Tundu Lissu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda, amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine vya siasa nchini, kuacha kumjadili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kwa kuwa amekiri bado hajapona na hivyo hakumbuki chochote.

“Siridhishwi na mjadala unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu Lissu." amesema Makonda.

Wakati anazungumza na gazeti la Nipashe, Ijumaa, jijini Dar es Salaam, Makonda alikuwa anajibu mjadala uliokuwa bungeni juu ya ziara ya Lissu Ulaya na Marekani hivi karibuni ambapo mbunge mmoja alidai kuwa Lissu anazurura na kuwa tayari ameshapona.

Tundu Lissu mwezi Februari 2019, akiwa ziarani Marekani alidai kuwa siku aliyopigwa risasi ndio siku Rais Magufuli alikuwa akipokea ripoti ya makinikia.

"Na siku nashambuliwa masaa mawili kabla Rais alisema, huyu anayepiga kelele ni msaliti, tuko vitani na mtu anayetusaliti vitani wanajeshi huwa wanajua namna ya kumalizana (naye) huko," alieleza Lissu.

Mnadhimu huyo wa kambi ya upinzani bungeni pia alidai kuwa "kumbuka ripoti hiyo ilikuwa inakabidhiwa jijini Dar na Mkuu wa Mkoa alikuwa hayupo Dar, na naambiwa alikuwa Dodoma.

"Cha ajabu eneo ninaloishi hulindwana saa 24 na askari wenye silaha lakini walinzi hao hawakuwepo kabisa katika viunga vya Area D.

Lakini hao Polisi wanaotaka kunihoji mimi hawajawahi kumwita wala kumhoji Makonda akiwa kama mshukiwa," alisema Lissu.

Lissu pia ameuliza kwa nini mtu aliyesema anafaa kufa hajawai kuulizwa juu ya kauli yake.

Kadhalika Lissu amehoji kwa nini askari waliotakiwa kuwa lindoni hawajawai kuulizwa walikuwa wapi siku ya tukio na nani aliwapa amri waondoke.

Makonda katika mahojiano na Nipashe alisema kuwa, kama Lissu hajapona, hawezi kurudi nchini kuwashukuru Watanzania na chama chake kilichomchangia fedha za matibabu.

"Nawasihi wanasiasa, vyama vya siasa, hasa chama changu CCM na Watanzania wazalendo, kuacha kumjadili na kumlaumu Lissu kwa sababu yoyote ile kwa sababu ameshathibitisha kuwa bado hajapona vizuri," Makonda alisema.

"Kama mgonjwa hajapona, ni wazi kuwa hawezi kukumbuka chochote, hawezi kurudi nchini kuwashukuru Watanzania na wananchi wake waliokuwa wakimwombea na kumtolea mchango.

"Lakini pia ni wazi kuwa hakumbuki chochote kama alichangiwa na akapatiwa matibabu mjini Dodoma. Hawezi kukumbuka hata maombi aliyofanyiwa na viongozi wa dini.”

Alidai kuwa wanasiasa na watu wanaomjadili na kumlaumu Lissu, hawapaswi kufanya hivyo kwa kuwa hana anachokumbuka kuhusu kilichomkuta na badala yake waendelee kumwombea arudi katika hali yake ya kawaida.

Makonda alidai Lissu hawezi kufahamu madhara yanayoipata nchi kwa kile anachokizungumza anapokuwa mataifa mengine kwa kuwa bado hajapona vizuri.

Alidai kuwa Watanzania ambao wataendelea kubishana na mbunge huyo juu ya kile anachozungumza, wataonekana wao ndiyo wenye matatizo.

Makonda aliwataka wanasiasa na wadau wa maendeleo kujikita kujadili masuala ya maendeleo na kuhoji ahadi zilizotolewa na serikali kuhakikisha taifa linapiga hatua kubwa za kukuza uchumi wake.

Alisema kuna miradi mikubwa inayoendelea nchini ikiwamo ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi mkubwa wa kufua umeme (Stiegler's Gorge) ambayo inatakiwa kufuatiliwa kwa karibu na wananchi.

"Wanasiasa na jamii wahoji utekelezaji wa miradi kama hii ya maendeleo badala ya kuendelea kupigia kelele suala Lissu ambaye bado yupo nje ya nchi kwa matibabu,” Makonda alisema.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, Lissu (51), amekuwa nje ya mipaka ya Tanzania akipatiwa matibabu kutokana na kushambuliwa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya gari lake nyumbani kwake Area D jijini Dodoma Septemba 7, 2017.

Baada ya shambulio hilo, mtaalamu huyo wa sheria alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alikopatiwa matibabu ya awali kisha kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya na baadaye Ubelgiji.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC

XS
SM
MD
LG