Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Oktoba 12, 2024 Local time: 03:51

Jumuiya ya kimataifa yashtushwa na tamko la Makonda


Balozi Michelle Bachelet
Balozi Michelle Bachelet

Balozi wa Umoja wa Mataifa anaye simamia Haki za Binadamu Michelle Bachelet Ijumaa amesema ameshtushwa na tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwamba kuna kamati itakayo undwa kufuatilia na kuwakamata mashoga, na kuwahamasisha watu kuripoti wale wanaoshukiwa kuwa mashoga.

“Watu wajinsia moja wanaofanya mapenzi nchini Tanzania tayari wamekuwa wanakabiliwa na ongezeko la uvunjifu wa amani, kubughudhiwa na kubaguliwa kwa kipindi cha miaka 2,” Balozi Bachelet amesema. “Na wale wanaojitetea haki zao kupata huduma za afya, kuishi maisha huru yasiyo kuwa na ubaguzi, uvunjifu wa amani na kukamatwa bila hatiya wameendelea kulengwa na hata kukamatwa.”

“Hili limegeuka kuwa ni kumtafuta mchawi na inaweza kutafsiriwa kama ni leseni ya kuendesha vitendo vya uvunjifu wa amani, kunyanyasa, kubughudhi na kuwabagua wale wote wanaohisiwa kuwa ni mashoga.”

Lakini Tanzania imesaini Mkataba wa Kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa, Mkataba wa Kimataifa wa haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni, na Mkataba wa Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake, ambao umeweka wazi haki ya kila mtu kuwa huru bila kubaguliwa; kuwa huru na kuhakikishiwa usalama wake; kupewa haki sawa mbele ya sheria na kulindwa na sheria; kutumia faragha yake; kutoteswa wala kufanyiwa ukatili, kutofanyiwa vitendo vya kinyama au kudhalilishwa au kuadhibiwa; kuwa na haki ya huduma ya afya, na katazo la aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake, ikizitaka nchi zote kutokomeza unyanyapaaji na kuwahukumu kutokana na jinsia yao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam

Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amewatoa hofu jumuiya ya kimataifa pamoja na Watanzania na wanadunia kwa ujumla na kuwashauri kuwa ingekuwa vyema kupata taarifa kutoka kwenye chanzo chenyewe, kuhusiana na kusakwa na kukamatwa mashoga.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Sauti ya Amerika amelaumu kuwa jumuiya ya kimataifa imekuwa ikichukua taarifa kutoka kwa watu yumkini ni washirika au wana maslahi binafsi na jambo hili husika, na hivyo wanatengeneza mazingira ambayo siyo juu ya zoezi hili.

Serikali ya Tanzania iwajibike

Bachelet amesisitiza kuwa serikali ya Tanzania itekeleze wajibu wake wa kulinda haki za binadamu za wananchi wote katika ardhi yake, ikiwemo kuwawajibisha watu ambao wanahamasisha chuki na ubaguzi na wale wanafanya vitendo vya kuvunja sheria. Serikali inawajibika kuhakikisha kuwa wanaotetea haki za binadamu, waandishi wa habari na wanaotoa huduma ya afya wanaweza kufanya kazi zao muhimu, bila ya kudhuriwa au kubughudhiwa.

Mpango uliotangazwa na serikali unahusisha jaribio la kile kinachosemwa kuwa ni “kuwatibu” mashoga - kitendo kinacho laaniwa kama ni chenye madhara, kinyume cha maadili na hakina hoja ya kisayansi kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Naitaka serikali na wananchi wa Tanzania kusimamia haki za binadamu ya kila mtu nchini, bila ya kujali ni kina nani au wanawapenda,” Bachelet amesema. Viongozi wa kisiasa, kidini na wengine wanawajibu wakupambana na vitendo vya ukandamizaji venye misingi ya utambulishi na mwenendo wa kijinsia.

Balozi huyo pia ametaka kupitiwa tena sheria zinazo toa adhabu kwa watu wa jinsia moja walioridhia kuwa na mahusiano yakimapenzi.

Sheria ya Tanzania

Mkuu wa Mkoa huyo amesisitiza kuwa anafuata sheria ya nchi inayokataza tendo la kutembea na mtu kinyume cha maumbile.

“Sheria hiyo imeweka wazi kabisa kwamba mtu anayefanya hivyo akibainika na akithibitika ni kifungo cha maisha au jela miaka 30,” amesema.

Ameongeza kusema kuwa: “ nchi ya Tanzania haijakubali kwamba ni nchi inayokubali mashoga, na hata katika tamko la haki za binadamu, sisi hatujachukuwa ushoga ni sehemu ya haki za binadamu, vinginevyo sheria hii isingeweza kuwepo iwapo ushoga ni sehemu ya haki za binadamu.”

“Tuwaulize hao wanao tutangazia haki za binadamu, ni haki kutusambazia mambo yenu ya faragha. Kwa sababu sasa hivi kama ninavyo ongea tayari kuna watu wamekwenda mahakamani, ambao wao wamefanyiwa kinyume cha maumbile, hawakuridhika wakaamua kujiripoti....”

Amekemea wale wanaotetea watu wanaoharibu kizazi, akisema ingekuwa ni vyema jambo lako la faragha libaki kuwa la faragha.

“Na ndiyo vita iliyoko kati yetu na hawa watu, kwa nini msifanye mambo yenu faragha mnayofanya na mnayatangaza mpaka kwenye dunia kwa watu ambao hawahusiki,” “Kwa nini mnataka watoto wetu waone mambo yenu ambao hawako hata katika umri wa kujua mambo hayo, amehoji Makonda.

Watu 47,000 watuma taarifa za mashoga

Makonda amesema mpaka Ijumaa wananchi wasiopunguwa 47,000 wametuma taarifa juu ya matokeo mbalimbali.

“Zoezi hili haliko kwa ajili ya kumwinda mtu au kumharibia mtu heshima yake, na ndio maana taarifa zote tulizopewa kama serikali bado zinafanyiwa kazi, na wale wanaotaja majina wataitwa kwenye vituo vya polisi, kuja kufafanua.”

Mkuu wa Mkoa amesema kuhusu zoezi la kupimwa: “Watu wanataka kwenda kupimwa kwa sababu mpaka hivi sasa tunavyo ongea kuna takriban mashoga wasiopungua 200 wanaotaka kuacha biashara hiyo ya ushoga na wanaomba msaada."

Ameeleza kuwa tayari mkoa umeandaa timu ya madaktari pamoja na wanasaikolojia wakiwasaidia kuwapa ushauri nasaha ili watoke kwenye kundi hilo la ushoga.

XS
SM
MD
LG