Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 22, 2024 Local time: 11:12

Siku ya Wafanyakazi Duniani : Serikali zatakiwa kuboresha hali ya maisha


Uhuru Kenyatta
Uhuru Kenyatta

Leo ni Siku ya Wafanyakazi Duniani. Wafanyakazi wote wanaadhimisha Mei Mosi kwa kuandamana na kutoa salamu za pamoja zenye ujumbe unaotaka serikali kuboresha hali zao za maisha.

Kauli mbiu 2019

Mwaka 2019 kauli mbiu ni ''Pensheni ya Kudumu kwa wote: Wajibu wa Ushirika wa Kijamii''. Wafanyakazi wakishirikiana na vyama vyao huadhimisha siku hii kwa kuandaa mipango mbalimbali itakayosaidia kuboresha mishahara ya wafanyakazi pamoja na mazingira bora ya kazi.

Mandamano mbalimbali yamefanyika pia katika nchi za Afrika Mashariki. Wafanyakazi nchini Kenya wanaeleza kukerwa na hatua ya serikali ya Kenya kutowapa nyongeza ya mshahara wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi jijini Nairobi, Jumatano.

Waandamanaji wakamatwa Kampala

Polisi mjini Kampala, Uganda, wamewakamata waandamanaji watatu, ambao walikuwa kati ya kundi la watu lililopinga maadhimisho ya siku ya wafanyakazi, yaliyofanyika katika wilaya ya Agago, iliyo kaskazini mwa nchi hiyo, na kuongozwa na Rais Yoweri Museveni.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, waandamanaji hao walikuwa wanaeleza kutoridhika kwao na gharama ya juu ya maisha, ambayo, walisema, imepelekea baadhi ya wafanyabiashara kufunga maduka yao. Wengi wao walisema hawakuona haja ya maadhimisho hayo.

Katika hotuba yake, Rais Museveni amesema kwamba utawala wake utaendelea kuwekeza kwenye sekta za uchukuzi na uzalishaji wa umeme, ili kuimarisha mazingira ya kufanya biashara, na kuwavutia wawekezaji.

Tamko la serikali

Serikali ya Kenya, imesitisha uamuzi wa kuwapa nyongeza ya mshahara wafanyakazi nchini humo hadi baada ya mashauriano na wadau husika. Hata hivyo, ni dhahiri serkali ya Kenya imejikuta katika mgogoro unaovuma kati ya muungano wa waajiri na muungano wa kutetea maslahi ya wafanyakazi.

Wafanyakazi walikuwa na matumaini mengi ya kupata nyongeza ya mshahara kipindi ambapo bidhaa za kimsingi zinapatikana kwa gharama ya juu nchini Kenya.

Rais Kenyatta

Pamoja na kuwa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Naibu wake walikosa kuhudhuria hafla hii, wafanyakazi walifika katika uwanja huu wa maadhimisho kutaka kufahamu mkakati wa serikali ya Kenya kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi kipindi ufisadi unaripotiwa zaidi katika taasisi za serikali. Aidha, serikali inawataka wafanyakazi wake wote kulipia ushuru wa asilimia 1.5% katika ujenzi wa makao bora kwa kila mwananchi.

Muungano wa waajiri

Lakini maadhimisho haya yanajiri wakati muungano wa waajiri nchini Kenya FKE umetangaza kutoridhia hatua yoyote ya serikali kuwapa wafanyakazi nyongeza ya mshahara.

Muungano huo Jumanne wiki hii ulikariri kuwa hatua yoyote ya kuwapa nyongeza wafanyakazi katika kipindi hiki ambapo uchumi wa Kenya umepondwapondwa, itaongeza migogoro kazini kati ya waajiri na wafanyakazi. Aidha, Muungano huo pia ulieleza kuwa haifai hafla ya maadhimisho kugeuzwa na kuwa siku ya kuwapa wafanyakazi nyongeza.

Muungano wa wafanyakazi

Lakini Muungano wa kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini Kenya COTU kupitia katibu wake mkuu Francis Atwoli, uliitaka serikali kuwaongezea wafanyakazi nyongeza ya asilimia 15% kuwakinga dhidi ya mkwamo wa uchumi. COTU inaeleza kuwa imeingia makubaliano serikali ya Rais Kenyatta kuwapa wafanyakazi nyongeza ili serikali itekeleze mfumo wake wa kutaka wafanyakazi wote kutoa ushuru wa asilimia 1.5% kufadhili ujenzi wa nyumba, hiyo ikionekana kuwa chambo cha kusuluhisha mgogoro huo.

Msimamo ambao chama cha Walimu KNUT iliuunga mkono ili kuwaepusha wakenya hali ngumu ya maisha jinsi anavyoeleza Wilson Sossion, Katibu Mkuu wa Chama hicho.

Lakini Wakenya walipata mshtuko wakati Waziri wa Kazi Ukur Yattani aliposisitiza kuwa bado hayapo makubaliano ya kutangaza nyongeza ya mshahara.

Ushauri kati ya waajiri

Bado tupo katika mashauriano kati ya waajiri na waajiriwa mbele ya baraza la kutathmini mishahara ya wafanyakazi. Mashauriano yanaendelea. Na iwapo patakuwapo nyongeza ya mshahara, hilo tutalijadili kabla ya wiki kukamilika, alieleza Waziri.

Ni usemi ambao uliwashtua Wakenya waliofika bustani ya Uhuru kutaka kujua iwapo serikali yao itawapa nyongeza ya mshahara.

Nyongeza ya 2018

Mwaka 2018, Serikali ya Kenyatta iliwapa wafanyakazi wenye malipo ya chini mno nyongeza ya asilimia 5% na vile vile kuvitaka vyama vya wafanyakazi nchini Kenya kukumbatia mazungumzo kupata suluhu kwa matatizo yanayovikumba

Mwaka 2017 Rais Kenyatta aliwapa wafanyakazi nyongeza ya asilimia 18% kupunguza makali ya mfumuko wa bei za bidhaa.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG