Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 11:59

Rais wa mali ajadiliana kuunda serikali mpya


Rais Ibrahim Boubacar Keïta
Rais Ibrahim Boubacar Keïta

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita, ameanza mazungumzo ya kuunda serikali mpya baada ya Waziri Mkuu Soumeylou Boubeye Maiga na serikali yake yote kujiuzulu hapo jana.

Taarifa kutoka ofisi ya rais inaeleza kwamba Rais Keita amepitisha kujiuzulu kwa waziri mkuu na mawaziri wake na kwamba atamtangaza waziri mkuu mpya pamoja na serikali baada ya mashauriano na vyama vyote vya kisiasa nchini humo.

Taarifa hiyo haikutoa sababu za kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Maiga. Inaaminika uamuzi huo unatokana na kuongezeka ghasia katika eneo la kati ya nchi hiyo, pamoja na mauwaji ya halaiki mwezi uliopita pale wafugaji 160 wa kabila la Fulani walipouliwa na wanoishkiwa kuwa ni wawindaji wa kabila la Dogon.

Umoja wa mataifa unaripoti kwamba mnamo mwaka mmoja uliopita mapigano kati ya wa-Fulani na wa-Dogon yamesababisha vifo ya wanawake, watoto na wanaume wapatao 600.

Wiki mbili zilizopita kulikuwa na maandamano makubwa katika mji mkuu wa Bamako kulalamika dhidi ya serikali kushindwa kukomesha ghasia nchini humo.

Mali imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya kurejesha uthabiti wa nchi tangu wanamgambo wa Kiislam wenye itikadi kali kuingia kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyodumu muda mfupi huko Bamako mwaka 2012, na kudhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Mali.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG