Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 20, 2024 Local time: 00:51

Wajue wagombea wakuu wa urais DRC


Wakazi wa DRC nchini Brazzaville.
Wakazi wa DRC nchini Brazzaville.

Katika mfululizo wetu wa Makala kuhusu uchaguzi mkuu wa rais Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, leo tunapata maelezo kuhusu wasifu wa wagombea wakuu kwenye kiti cha urais.

DRC inafanya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge Disemba 23. Mwenzetu Patrick Nduwimana anaangalia pia sera zinazowekwa mbele na wagombea hao.

Idadi ya wapiga kura

Zaidi ya raia wa congo millioni 46 watajielekeza kwenye vituo vya kura jumapili, kuwachagua wagombea u rais, wabunge kwenye ngazi ya taifa na majimbo. Wagombea kwenye kiti cha u rais wote pamoja ni 21 akiwemo mgombea moja mwanamke. Lakini hapa tunaangazia wasifu wa wagombea wakuu wa tatu ambao ni Emmanuel Ramazani Shadary, Martin Fayulu na Felix Tshisekedi, pamoja pia na sera zao za kisiasa.

Ramazani Shadary
Ramazani Shadary

Emmanuel Shadary:

Emmanuel Shadary ni mgombea wa muungano wa vyama tawala (FCC), aliteuliwa na Rais Joseph Kabila ambae haruhusiwi kuwania muhula mwengine kulingana na katiba ya jamhuri ya kidemokrasiya ya congo. Shadary aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani katika serekali ya Joseph Kabila. Kabla ya kuteuliwa kama mgombea wa chama tawala, alikua mbunge wa taifa.

Sera ya Shadary inazingatia mambo manne muhimu ambayo ni kuboresha uhasibu wa mali ya umma, kukuza uchumi unaozalishwa na rasilimali nyingi, kupambana na umaskini na kutowa ajira. Shadary anasema akichaguliwa, bajeti ya serekali yake katika kipindi cha miaka mitano itakua sawa na dola billioni 86. Anaahidi kutowa ajira laki moja kuanzia mwaka wa 2020.

Alipoanzisha kampeni yake katika mji wa Lumbumbashi hapo Novemba 26, Shadary alisema atawapa ajira vijana.

Martin Fayulu
Martin Fayulu

Martin Fayulu:

Martin Fayulu anasimamia kambi ya muungano wa upinzani, muungano uliopewa jina la “ Lamuka”. Fayulu alifanya kazi kwenye sekta ya biashara. Tangu mwaka wa 1984 hadi 2003, alifanya kazi kwenye kampuni ya mafuta ya marekani, Exxon Mobil. Baada ya kuachana na kampuni hiyo, alirejea nyumbani kumiliki kampuni zake. Kati ya mwaka wa 2006 na 2011, alikua mbunge wa taifa na wa mji wa Kinshasa.

Sera ya Fayulu inayapa kipaumbele mambo sita nyeti: utawala bora, mshikamano wa kitaifa, maendeleo ya kudumu, haki sawa kwa raia wote wa Congo, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kupata uraia unapotimiza masharti.

Fayulu amesema, atakaposhinda uchaguzi, ataipatia serekali yake bajeti ya dola billioni 105 katika kipindi cha miaka mitano.

Fayulu anapania pia kuifanyia marekebisho katiba ya nchi ili kuwepo uchaguzi wa duru mbili na haki ya kuwa na uraia pacha. Fayulu ameahidi pia kupiga vita ufisadi na kufanya mageuzi kwenye sekta ya sheria.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na sauti ya Amerika, Martin Fayulu amesema, kupambana na umaskini na kuendeleza biashara ni baadhi ya mambo atakayoshughulikia akifika madarakani.

“Nataka kuondowa umaskini katika jamii za wakongo, tunataka kutowa ajira kwa raia wa Congo, tunataka kuifanya congo iwe nchi ambayo inavutia wawekezaji na wafanyabiashara.”

- Felix Tshisekedi
- Felix Tshisekedi

Felix Tshisekedi:

Felix Tshisekedi ni mwanae hayati Etienne Tshisekedi. Mwaka wa 2016, aliteuliwa kama katibu mkuu wa chama cha UDPS kilichokua kinaongozwa na baba yake. Felix Tshisekedi aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la Mbuji Mayi mwaka wa 2011.

Felix Tshisekedi alikuwa na nafasi ya mbele kama mpinzani, kwenye mazungumzo ya kutafuta mkataba wa kuanda uchaguzi, mazungumzo yaliyosimamiwa na kanisa katolika la jamhuri ya kidemokrasiya ya congo. Mkataba huo kati ya wanasiasa wote wa DRC ulipatikana tarehe 31 disemba mwaka wa 2016, baada ya Rais Joseph Kabila kushinikizwa na wapinzani wake walioitisha mara kadha maandamano ya kumtaka aache madaraka na aandae uchaguzi.

Tshisekedi anapania kukuza uchumi wa nchi na kuongeza mapato ya wanainchi wa Congo. Amesema atakapochukua hatamu za uongozi, ataongeza mapato ya mwananchi wa congo kutoka dola 1 na senti 25 kwa siku, sawa na dola 458 kila mwaka, hadi dola 11 na senti 75 kwa siku, sawa na dola 4288 kila mwaka.

Anasema bajeti ya serekali yake itakua ya dola billioni 86.7 katika kipindi cha miaka mitano.

Tshisekedi anashirikiana na mpinzani mwengine Vital Kamerhe, baada ya wote wawili kujiondowa kwenye muungano Lamuka unaojumuisha wapinzani vigogo kama Jean Pierre Bemba na Moise Katumbi na kuongozwa na Martin Fayulu.

Tshisekedi na Kamerhe walipozinduwa kampeni yao katika mji wa Goma disemba 14, walisema watafanya marekebisho kwenye sekta ya madini, ili wanainchi wa congo wanaufaike zaidi na uzalishaji wa madini kuliko ilivyo hivi sasa.

Hitimisho

Uchaguzi wa jumapili iwapo utafanyika kwa amani na utilivu, na iwapo utakua huru na wa haki, bila shaka congo itakua imepiga hatua kubwa kwa kumaliza migogoro ya kisiasa ya zaidi ya miongo miwili, iliosababisha mafaa mengi, wimbi la wakimbizi, kudorora kwa uchumi na umaskini miongoni mwa raia wa DRC.

XS
SM
MD
LG