Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 10:01

Rais Samia amsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Bandari


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, ili wapishe uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha bandarini.

Rais ametoa uamuzi huo Jumapili, baada ya kukabidhiwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ikulu ya Chamwino, Dodoma, inayobaini kuna ubadhirifu wa karibu shilingi bilioni nne za Kitanzania katika shirika la bandari,

“Ripoti nimeiona, nimeipitia na imebaini ubadhirifu mkubwa uliofanywa pale bandari, hili suala mnatakiwa kushirikiana, nakuomba Takukuru jishughulishe pale, alipita Waziri Mkuu alilishughulikia.

“Waziri Mkuu aliunda kamati na wakafanya uchunguzi kidogo, hatua chache zilichukuliwa lakini imani yangu ni kwamba kama kuna ubadhirifu pale waliosimamishwa ni hawa wa chini, ninaomba mara moja nitoe agizo la kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa Bandari halafu hatua zaidi ziendelee,” amesema Rais Samia.

Rais pia amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo kufuatilia upotevu wa fedha katika ofisi yake na endapo atashindwa kufanya hivyo atoe taarifa asaidiwe.

Rais amesema hayo baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na ripoti ya TAKUKURU ya 2019/2020, Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma, ambapo ripoti ya CAG ilionyesha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, alikagua hati 185 ambapo hati zinazoridhisha ni 124, hati zenye mashaka ni 53 na hati mbaya 8.

“TAMISEMI kuna upotevu mkubwa wa fedha, Waziri Jafo uko hapa tunaomba uhangaike mara ya mwisho ukishindwa sema tukusaidie, Tamisemi mnachukua fedha nyingi serikali kuu lakini wao hawarudishi,” alisema Rais Samia.

Awali akisoma ripoti yake mbele ya Rais Samia, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Charles Kichere amesema kuwa hali ya utekelezaji wa mapendekezo anayotoa kwa serikali bado hairidhishi kwani asilimia 30 pekee ya mapendekezo ndio yamefanyiwa kazi, hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuimarisha na kuongeza mapato kwa kudhibiti mifumo ya ndani.

“Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 nimetoa jumla ya hati 900 za ukaguzi ambapo nimetoa kwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Miradi ya Maendeleo, Mashirika Binafsi pamoja na Vyama vya Siasa, kati ya hizo hati zinazoridhisha ni 800 sawa na 89% hati zenye shaka ni 81 sawa na 9% mbaya 10 sawa na 1%”, imebainisha ripoti ya CAG Charles Kichere.

XS
SM
MD
LG