Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:10

Mkuu wa IMF huenda akapewa dhamana


Dominique Strauss Kahn akifikishwa mahakamani New York
Dominique Strauss Kahn akifikishwa mahakamani New York

Mawakili waahidi dhamana ya dolla millioni moja na mkanda wa eletroniki utakaoonyesha alipo wakati wote

Mawakili wa Mkuu wa shirika la IMF, Dominique Strauss-Kahn, ambaye anashikiliwa rumande kwa madai ya ubakaji wamewasilisha rufaa mpya Jumatano ya kutaka atolewe kwa dhamana kutoka katika gereza la Rikers Island.

Katika ombi hilo jipya la rufaa Strauss-Kahn yuko tayari kuweka dhamana ya dolla millioni moja fedha taslimu, kutotoka nyumbani kwa binti yake Manhattan huku akiwa na mkanda wa elektroniki ambao utaonyesha kila alipo wakati wote, na kukabidhi hati zake za kusafiria za Umoja wa Mataifa. Rufaa hiyo imesema Strauss-Kahn ambaye ni raia wa Ufaransa tayari amekabidhi pasi yake ya kusafiria.

Habari za kuaminika zimesema Jumatano kuwa mashauriano yanaendelea ambapo huenda akatolewa kwa dhamana Alhamisi. Mashauriano hayo yako katika hatua za awali na hakuna hakika kama yatafanikiwa.

Rufaa hiyo ya dhamana imewasilishwa katika mahakama kuu ya jimbo la New York na itasikilizwa Alhamisi. Rufaa hiyo inaelezea pia kuwa Strauss-Kahn ana mke wa zaidi ya miaka 10 na ana watoto wanne kutoka katika ndoa ya awali, mmoja wa binti yake anaishi New York ambako ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Columbia.

Wakati huo huo, mwanamke raia wa Guinea ambaye ndio chanzo cha mashitaka dhidi ya Strauss-Kahn alitazamiwa kutoa ushahidi mbele ya jopo la wazee wa mahakama Jumatano ambalo litaamua endapo kuna kesi ya kufunguliwa Strauss-Kahn ama la.

Mwanamke huyo, mjane anayeishi na binti yake wa miaka 15 katika eneo la Bronx mjini New York, atakanusha madai yoyote ya kuwa alifanya ngono kwa kuelewana na Strauss-Kahn.

Amekuwa akifanya kazi katika hoteli hiyo kwa miaka mitatu na maafisa wa hoteli wanasema ni mfanyakazi mzuri.

XS
SM
MD
LG