Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Julai 17, 2024 Local time: 18:34

Mkutano wa chama cha upinzani UNITA waanza, kiongozi wake ajiuzulu


Wafuasi wa UNITA wakati wa mkutano wa kampain Luanda Augusti 25, 2012
Wafuasi wa UNITA wakati wa mkutano wa kampain Luanda Augusti 25, 2012

Mkutano wa chama cha upinzani Unita umeanza Jumatano ambapo kiongozi wa chama cha hicho Isaias Ngola Samakuva, ataachia uongozi wa chama hicho baada ya kukitumikia kwa miaka 16.

Samakuva mwenye umri wa miaka 73 alichukuwa uongozi wa UNITA mwaka 2003 mwaka mmoja baada ya kuuliwa kwa muasisi wa chama hicho Jonas Savimbi.

Mchakato wa kumchagua mrithi wake utafanyika siku ya Ijumaa, na hivyo huu utakuwa mkutano wake wa mwisho kuongoza.

Akizungumza na shirika la habari la AFP kabla ya mkutano mkuu wa chama chake Jumatano, kiongozi huyo amesema chama chake kimefanya mageuzi makubwa kuweza kuwavutia wapiga kura na atakae chukua nafasi yake ataweza kukiongoza chama hadi ushindi katika uchaguzi ujao.

“UNITA ilikuwa katika vita, lakini baada ya Dk. Savimbi kuuawa, haikua jambo rahisi kuchukua uongoizi , kukipanga upya chama na kukifanya UNITA chama cha kisiasa namna ilivyo hii leo.’ Amesema Samakuva.

Chama hicho kilichokuwa kikundi cha waasi hapo awali hakijawahi kushinda uchaguzi tangu Samakuva kukibadilisha na kuwa chama kikuu cha upinzani 2003.

Taifa hilo la kusini magharibi ya Afrika lenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi limekuwa likiongozwa tangu uhuru wake kutoka Ureno 1975 na Chama cha Ukombozi cha Angola, MPLA.

Akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa mkutano mkuu wa chama chake cha UNITA Samakuva anasema anatambua changamoto kubwa inachokikabili chama hicho hivi sasa.

“Changamoto kuu tulionayo ni kushinda katika uchaguzi hivi sasa na nina matumaini ya dhati kwamba katika muda wa miaka mitatu ijayo wakati wa uchaguzi mkuu, UNITA inaweza kuchukuwa madaraka, hiyo inawezekana. Amesisitiza Samakuva

Katika uchaguzi uliyopita mwaka 2017 UNITA ilipata asilimia 26 za kura ikiwa nafasi ya pili mbali na chama tawala cha MPLA kilichopata asili mia 61 za kura. Licha ya kushindwa huko Samakuva yungali na matumaini.

“Chama cha MPLA hakina tena nguvu kama ilivyokuwa awali, kwa maoni yangu, UNITA kimepanuka na kuongeza ushawishi wake kote nchini,” akiongezea kwamba wanachama wake wameongezeka kutoka 900,000 mwaka 2002 hadi zaidi ya milioni tatu hivi leo.

Samakuva tayari alitangaza kwamba atachia uongozi wa chama baada ya uchaguzi wa 2017, pale rais wa zamani Jose Eduardo dos Santos alipoachia madaraka baada ya miaka 38.

Aliyechukua nafasi yake Joao Lourenco amefanya mageuzi makubwa pamoja na kupambana na ulaji rushwa na Samakuva anakiri kwamba amepunguza ukosoaji tangu Lourenco kuchukua madaraka.

“Rais Joao Laurenco amejaribu kubadili namna anavyotawala kulingana na aliyemtangulia. Ana malengo kadhaa mazuri lakini hali hapa ni kwamba mambo ni magumu sio tu kiuchumi bali pia kijamii, ambayo ninadhani inampatia shida kutekeleza malengo yake."

Licha ya utajiri wa mafuta, gesi naakiba ya madini sehemu kubwa ya wa-Angola wanaishi katika umaskini na wanaendelea kutegemea katika kilimo cha kukidhi mahitaji yao.

Wajumbe wa UNITA wanaanza mkutano wao mkuu Jumatano na wanatarajia kumchagua kiongozi mpya siku ya Ijuma.

Kuna wagombea watano wanaopigania nafasi hiyo, akiwemo kiongozi wa UNITA bungeni Adalberto Costa Junior na makamu rais wa chama Raul Danda.

Samakuva anasema mtu anaestahiki kuchukua nafasi yake ni yule atakae hakikisha anaendelea na kile alichokianzisha na kuwa na nguvu na busara kuweza kuleta ushindi.

Amesisitiza kwamba ana matumaini makubwa UNITA kitachukua madaraka wakati wa uchaguzi wa 2022.

UNITA kiliundwa wakati wa vita vya uhuru vya angola 1966, na kwa muda mrefu kimeambatanishwa na kiongozi wake muasisi Savimbi aliyekuwa na uongozi wa kimabavu.

Baada ya uhuru Angola ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 27 na kusababisha vifo vya watu nusu milioni.

XS
SM
MD
LG