Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 29, 2022 Local time: 08:13

Mapendekezo ya marekebisho ya katiba Kenya yachukua sura mpya


Rais Uhuru Kenyatta kushoto na Makamu wa Rais William Ruto

Kutangazwa kwa mapendekezo ya marekebisho ya katiba nchini Kenya kupitia ripoti ya jopo la maridhiano maarufu kama BBI ili kupanua serikali, kunaendelea kupokea hisia mbalimbali na maoni mseto kutoka kwa raia wa Kenya, makundi na mashirika mbalimbali. 

Viongozi walioonekana kupinga ripoti ya awali ya jopo hilo sasa wanaonekana kubadilisha msimamo na kutaka pawepo na maelewano ya wote kuhusu ripoti hiyo wanayosema inajaribu kutoa suluhu kwa matatizo ya nchi hiyo.

Hatua hii inaashiria kuwa Kenya huenda ikawa na serikali inayojumuisha rais, makamu wa rais, waziri mkuu, manaibu wake wawili wanaoteuliwa na kufutwa kazi na rais. Pia wabunge 360 kutoka bunge la taifa, 94 kutoka bunge la Seneti na vile vile kuondoa kabisa nafasi za wawakilishi wanawake 47 kama inavyopendekezwa katika ripoti ya jopo la maridhiano, ni suala linaloendelea kuibua hisia na maoni mseto kutoka kwa raia wa Kenya.

Bunge la Kenya
Bunge la Kenya

Mapendekezo haya katika ripoti hii yanaipa Kenya sura mpya katika uongozi kwani manaibu wa waziri mkuu wawili watahudumu kuwa mawaziri. Wakati Waziri Mkuu atawajibikia vitendo vya serikali bungeni.

Mapendekezo haya yanatajwa kuwa ni jumuishi na yenye lengo la kuondoa mtindo wa urais “mshindi ndiye anayechukua kila kitu” na anayeshindwa kubaki bila chochote. Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto awali alionekana kupinga marekebisho ya katiba yanayowapa watu wachache madaraka. Lakini sasa inaripotiwa kuwa anaonekana kulegeza msimamo na mtazamo wake.

Pia, wabunge wanaomuunga mkono katika azma yake ya kuwania urais ifikapo mwaka 2022 wameonekana kulegeza msimamo huo huku wakitaka wote kujumuishwa katika mdahalo wa taifa kuhusu ripoti hiyo.

Awali wabunge wa bunge la taifa wakiongozwa na Kiongozi wa shughuli za serikali bunge humo Amos Kimunya wameeleza kuwa wanaunga mapendekezo yalio kwenye ripoti hiyo hasa yanayokinga usawa wa kijinsia, suala ambalo lingali kaa la moto.

Pia chini ya marekebisho hayo biashara ndogondogo za vijana zitapata msamaha wa miaka saba kutolipia biashara hizo kodi ili kuziwezesha biashara hizo kukua na kupata usaidizi wa kifedha kutoka serikalini.

Ili kupambana na ufisadi, ripoti hii inapendekeza Benki Kuu ya Kenya kuondoa na kufuta leseni au kutoza adhabu nzito kwa benki na wakuu wake iwapo itapatikana benki fulani imehusika katika utakatishaji wa fedha haramu.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG