Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 22:19

Tanzania yazuia safari za Kenya Airways nchini mwake


Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways ikitua Nairobi
Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways ikitua Nairobi

Tanzania imesimamisha shirika la ndege la Kenya (KQ) kufanya safari za kwenda Tanzania kuanzia August 1, siku moja baada ya Kenya kutangaza kuwa itafungua anga zake kwa usafiri wa kimataifa isipokuwa kutoka baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania.

Katika barua kwa KQ Ijumaa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya safari za anga Tanzania (TCAA), Hamza S. Johari, alisema serikali ya Tanzania imesimamisha safari za KQ kati ya Nairobi na viwanja vya Tanzania kama Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar mpaka itakapotangazwa tena kujibu hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya.

Ijumaa serikali ya Kenya ilitangaza kufungua anga zake kwa safari za ndege za kimataifa baina ya Kenya na nchi mbali mbali zikiwemo nchi jirani za Ethiopia, Uganda na Rwanda isipokuwa Tanzania.

Tanzania na Kenya zimekuwa katika mvutano tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona ambapo mwezi Mei nchi hizo zilifungiana mipaka kwa muda mfupi kwa madai ya kuambukizana virusi vya corona. Hatua hiyo ilitatiza usafiri wa mizigo baina ya nchi hizo kwa wiki kadha mpaka zilipokubaliana kuhusu utaratibu wa kupima madereva wa malori ya mizigo.

Tangu mwezi Aprili Tanzania haijatoa idadi ya maambuziki ya Covid-19 nchini mwake na Rais John Magufuli amekaririwa mara kadha akisema hakuna tena corona nchini humo.

Kwa upande wake Kenya imekuwa ikipambana na maambukizi ya Covid-19 na hata kufunga shughuli katika baadhi ya miji mikubwa ya nchi hiyo. Wiki hii Kenya ilitangaza hatua nyingine kadha katika jitihada za kupunguza maambuziki na hadi Ijumaa ilikuwa imetangaza maambukizi zaidi ya 20,000.

XS
SM
MD
LG