Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 10, 2023 Local time: 20:18

Ethiopia yawafukuza wanadiplomasia wanne wa Ireland


Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Ethiopia imewafukuza wanadiplomasia wanne wa Ireland kwa sababu ya msimamo wa Ireland kuhusu mzozo unaoendelea katika taifa hilo la Pembe ya Afrika. 

Wanne hao wamepewa wiki moja kuondoka, taarifa kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland Simon Coveney ilisema.

Balozi na mfanyakazi mmoja wa ubalozi hata hivyo wameruhusiwa kubaki nchini.

Waziri huyo alisema kuwa mamlaka za Ethiopia zilieleza kuwa kufukuzwa huko ni kwa sababu ya msimamo wa Ireland kuhusu mzozo na mgogoro wa kibinadamu ambao umewaacha mamilioni ya watu wakihitaji msaada wa haraka wa chakula.

Alisema anajutia hatua hiyo lakini ubalozi huo utaendelea kuwa wazi. Ireland imekuwa na ubalozi nchini Ethiopia tangu 1994.

Nchi hiyo, ambayo inashikilia kiti kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, imekuwa ikikemea ukatili uliofanywa na pande zote mbili katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka mmoja uliopita.

Baadhi ya maafisa wa UN walifukuzwa mwezi Septemba wakati wengine karibu watano bado wako jela.

Hakuna sababu yoyote iliyotolewa kutokana na kukamatwa kwao. Katibu mkuu wa UN Antonio Guterres ametoa wito wa kumalizika haraka mapigano nchini Ethiopia.

XS
SM
MD
LG