Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 10:54

Kenya na Afrika kusini zinatoa wito kwa pande zinazopingana Ethiopia kusitisha mapigano


Rais C. Ramaphosa wa Afrika Kusini na Rais U. Kenyatta wa Kenya wazungumza na waandishi habari.
Rais C. Ramaphosa wa Afrika Kusini na Rais U. Kenyatta wa Kenya wazungumza na waandishi habari.

Rais Ramaphosa na Rais Kenyatta wamesema Jumanne kwamba wanaamini bado kuna nafasi ya mazungumzo kwa pande zinazozozana nchini Ethiopia na kuna umuhimu mkubwa kwa pande zote katika mzozo huo kukubaliana kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya kisiasa yenye maslahi kwa wote

Afrika Kusini na Kenya Jumanne imezihimiza pande zote zinazogombana nchini Ethiopia kukubaliana juu ya kusitisha mara moja mapigano, siku moja baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuapa kwamba atakwenda kwenye uwanja wa mapigano kuongoza wanajeshi wanaopambana na waasi. Wito huo umetolewa wakati wa mazungumzo kati ya Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa na mgeni wake Rais Uhuru Kenyatta ambaye yuko ziarani Afrika Kusini.

Rais Ramaphosa na Rais Kenyatta wamesema katika mkutano wa waandishi wa habari nje ya ikulu mjini Pretoria kwamba wanaamini bado kuna nafasi ya mazungumzo kati ya pande zinazozozana nchini Ethiopia na kwamba kuna umuhimu mkubwa kwa pande zote katika mzozo huo kukubaliana juu ya kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya kisiasa yanayohusisha pande zote.

Kabla ya kuanza mkutano na waandishi habari mawaziri wa nchi hizo mbili wametia saini makubaliano kadha ya maelewano kuhusu ushirikiano kati ya nchi zao mbili.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Rais Kenyatta yuko katika ziara rasmi ya siku mbili nchini Afrika kusini ili kuchunguza maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara na uwezekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Marais hao wanajadili pia suala la utengenezaji na usambazaji wa chanjo ya COVID-19 barani Afrika.

Kenyatta atakitembelea kesho Jumatano kiwanda cha kutengeneza dawa cha Aspen Pharmacare kinachopatikana katika mji wa Gqeberha uliokua ukijulikana kama Port Elisabeth ili kujionea utengenezaji wa chanjo za Johnson and Johnson za COVID-19. Kiwanda hicho kina uwezo wa kutengeneza dozi millioni 220 za Johnson and Johnson kwa mwaka, nyingi kati ya dawa hizo zinasafirishwa katika nchi za Afrika.

Kenya ni mmoja wa washirika wakuu wa kibiashara wa Afrika kusini barani Afrika nje ya Jumuia ya maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika kusini
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika kusini

Afrika Kusini ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola millioni 500 hadi Kenya mwaka 2020 ikilinganishwa na uagizaji wa bidhaa zenye thamani ya dola millioni 22 kutoka Kenya kulingana na takwimu rasmi. Zaidi ya makampuni 60 ya Afrika kusini yanaendesha shughuli mbali mbali nchini Kenya.

XS
SM
MD
LG