Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 22:23

Burundi : Uchaguzi wafanyika wakati mlipuko wa corona ukiendelea


Wapiga kura wa Burundi wakisubiri kupiga kura ya kumchagua rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa mji Gitega, Burundi May 20, 2020. REUTERS/Evrard Ngendakumana
Wapiga kura wa Burundi wakisubiri kupiga kura ya kumchagua rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa mji Gitega, Burundi May 20, 2020. REUTERS/Evrard Ngendakumana

Zaidi ya watu milioni tano ambao wanastahili kupiga kura katika nchi ya Afrika Mashariki ya Burundi wanapiga kura Jumatano kumchagua mrithi wa Rais wa muda mrefu Pierre Nkurunziza, vimeeleza vyanzo mbalimbali vya habari. 

Nkurunziza anaachia madaraka baada ya kuongoza kwa miaka 15, miaka mitano ya mwisho iliyokuwa na machafuko baada ya kuendelea na muhula wa tatu uliopata upinzani na kusababisha vifo vya watu 1 200 na zaidi ya raia 300,000 kukimbia machafuko katika nchi hiyo maskini.

Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, UN, unaonyesha kuwa mamia ya watu waliouawa wakati wa machafuko hayo walilengwa na vikosi vya serikali, tuhuma ambazo Burundi imezikanusha.

Wagombea saba wako katika kinyang’anyiro hicho cha kuchukua nafasi ya Nkurunziza, akiwemo Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye, mgombea aliyechaguliwa na rais, na mkuu wa upinzani Agathon Rwasa.

Makamu wa kwanza wa rais wa Burundi Gaston Sindimwo, anaegombania pia kiti cha rais kupitia chama cha UPRONA anapongeza jinsi uchaguzi umeendelea lakini anasema kuna kasoro kadha wa kadha zinatendeka.

Kura inayopigwa Jumatano inafanyika wakati kuna mlipuko wa virusi vipya vya corona nchini Burundi, ambapo hadi sasa watu 42 wameambukizwa na kifo kimoja katika nchi yenye takriban watu milioni 11.

Uongozi wa Burundi kwa kiasi kikubwa umepuuza hatari za virusi vya corona, na kuruhusu mikutano mikubwa ya kisiasa kufanyika hadi kufikia siku ya kupiga kura na kutoweka masharti yoyote juu ya mizunguko ya watu.

Mkuu wa Shirika la Afya, WHO, nchini Burundi alifukuzwa wiki iliyopita baada ya kueleza wasiwasi wake juu ya uelewa wa serikali unavyokinzana na hatari inayoletwa na virusi vya corona.

Hakuna waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi walioruhusiwa nchini Burundi kufuatilia upigaji kura baada ya serikali kusema mtu yoyote mgeni anayeingia nchini ataweka karantini kwa siku 14.

XS
SM
MD
LG