Upatikanaji viungo

Breaking News

Baraza la Kijeshi Sudan, vyama vya siasa, waandamanaji kuanza majadiliano Ijumaa


Waziri wa Ulinzi wa Sudan Awad Mohamed Ahmed Ibn Auf, mkuu wa baraza la kijeshi la mpito akishuhudia kuapishwa kwa Mkuu wa Majeshi, Lt. Jen. Kamal Abdul Murof Al-mahi ambaye anakuwa naibu wa baraza hilo.

Baraza la kijeshi la Sudan limetangaza Ijumaa kwamba linanaza majadiliano na vyama vya kisiasa pamoja na waandamanaji walioweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi na ikulu ya rais.

Tangazo hilo lilitolewa na kiongozi mpya wa baraza la mpito la kijeshi, Waziri wa Ulinzi wa serikali iliyopinduliwa, Awad Ahmed Ibn Auf, akizungumza na waandishi habari mara baada ya kuapishwa kuongoza serikali hiyo ya mpito.

Ibn Auf amesema rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir hatopelekwa katika mahakama ya uhalifu wa kimataifa ICC huko The Hague, lakini huwenda akafunguliwa mashtaka huko Sudan .

Ahmed Ibn Auf anakuwa rais mpya wa kipindi cha mpito wa sudan na mkuu wa majeshi Luteni Jenerali Kamal Abdul Murof Al-mahi anakua makamu wake.

Hata hivyo waandamanaji waliendelea kuweka kambi nje ya Ikulu siku moja baada ya kupinduliwa Bashir na kuendelea kuandamana jana usiku wakikaidi amri ya jeshi ya kutotoka nje usiku.

Katika mazungumzo yake na waandishi habari kiongozi huyo mpya amesema hawataruhusu waandamanaji kufunga barabara wala madaraja.

Ripoti zilizotufikia asubuhi ya leo kutoka Sudan zinasema kuwa watu walikuwa wanasherekea mabadiliko hayo kwa kupiga muziki katika mitaa ya Khartoum.

Wakati hayo yakiendelea viongozi wa mataifa ya kigeni wanapongeza mabadiliko huko Sudan, lakini wametoa wito wa kuwepo mabadiliko ya kidemokrasia kama vile wananchi wanavyotaka.

Marekani imetangaza uungaji mkono wa nguvu ya mageuzi ya amani ya kidemokrasia huko Sudan.

Naibu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje Robert Palladino anasema Marekani inatowa wito kwa viongozi wa kijeshi kuwaruhusu wananchi kueleza matakwa yao kwa njia ya amani.

Ameongeza kusema : "Wakati matukio yakiendelea kujitokeza tunatowa wito kwa wakuu wa utawala wampito kuonesha ustahmilivu na kuruhusu raia kushirika kwa nafasi katika masuala ya serikali. Tuna wapongeza wananchi wa Sudan kwa ukakamavu wao na dhamira yao ya kueleza matakwa yao ya haki bila ya kufanya ghasia.

Rais wa uturuki Recep Tayyip Erdogan mshirika mkuu wa Sudan amesema anamatumaini utaratibu wa kidemokrasia utarudi katika nchi hiyo.

Uchina nayo imesema inafuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea huko Khartoum.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG