“Ni kwa mara ya kwanza nimekuwa na hisia nzito – hilo linajitokeza,” amesema mwananchi wa Indonesia, 40, Sobar anahudhuria ibada hiyo kwa kutumia lugha nyepesi ya Kiarabu.
Zaidi ya mahujaji milioni 1.8 walikuwa wamewasili nchini Saudi Arabia siku ya Jumanne, serikali ya Saudia imesema.
Makundi ya waumini wa Kiislam kutoka dunia nzima walikuwa wamevalia nguo nyeupe za Hijja wakiwa wanateremka katika msikiti mtukufu ulioko magharibi wa nchi ya kifalme.
Mahujaji watatembelea maeneo matakatifu ambayo hayajabadilika tangu kuwasili kwa dini ya Kiislam karne 14 zilizopita.
“Uislam unatuunganisha. Sisi sote tuko pamoja… na ndiyo sababu ninafuraha,” amesema Leku Abibu, 46, fundi wa magari kutoka Uganda aliyekuwa amevalia kanzu iliyokuwa pana.
“Ninafurahia kuwa hapa.”
Ibada ya Hijja ya mwaka huu inafanyika wakati kukiwa na mgogoro katika eneo la Ghuba lililochangiwa na mtiririko wa mashambulizi ya meli za mafuta, mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani na kuzuiliwa kwa meli zinazosafiri baharini.
Saudi Arabia, nchi inayoongoza kijeshi katika Ghuba, na mshirika wake Washington wanaituhumu Iran –hasimu wa Riyadh katika eneo – kuwa imehusika na mashambulizi hayo na operesheni za hujuma dhidi ya meli za biashara.
Tehran imekanusha kuhusika.
Pamoja na kukosekana mahusiano ya kidiplomasia kati ya Saudi Arabia na Iran, mahujaji wapatao 88,550 kutoka Iran watashiriki katika ibada ya Hijja mwaka 2019, kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim.