“Watawala wanataka nchi yetu irudi kwenye chama kimoja,” amesema kiongozi wa ACT Wazalendo na mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe.
Wakati akiongea na Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA Ijumaa, ameongeza kuwa upinzani utaendelea kupambana na hali hiyo ili kuhakikisha kwamba wanazuia wimbi hilo la kuipeleka nchi katika chama kimoja.
Zitto Kabwe aliachiwa huru Ijumaa kwa dhamana. Zitto amesema kuwa alikamatwa na polisi usiku wa kuamkia Februari 23 mkoani Morogoro nchini Tanzania, wakidai kuwa alikuwa amefanya mikutano bila ya kibali.
Zito amefafanua alikamatwa akifanya ziara ya kutembelea viongozi wa chama chake cha ACT Wazalendo maeneo ya Morogoro.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Sunday Shomari, Washington, DC