Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 10:17

Wachezaji wa mpira wa vikapu Marekani wasusia michuano ya fainali


Watu wakiandamana kupinga kupigwa risasi mtu mweusi kwa jina la Jacob Blake katika mji wa Kenosha, Wisconsin.
Watu wakiandamana kupinga kupigwa risasi mtu mweusi kwa jina la Jacob Blake katika mji wa Kenosha, Wisconsin.

Wachezaji wa kulipwa wa mchezo wa mpira wa vikapu wanaume na wanawake hapa Marekani wamesusia wiki hii kushiriki kwenye michuano ya finali ambayo imekuwa ikiendelea wakilalamika dhidi ya polisi kumpiga risasi Jacob Blake Mmarekani Mweusi katika mji wa Kenosha, jimbo la Wisconsin mwishoni mwa wiki.

Shirikisho la kitaifa la mpira wa vikapu la wanawake WNBA liliahirisha mechi 3 Jumatano baada ya timu ya Washington Mystics kususia mechi yao dhidi ya timu ya Atlanta Dreams wakilalamikia dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Msimamo huo ulifuatia uamuzi wa awali wa shirikiso la wanaume NBA kusitisha michuano baada ya baadhi ya timu kususia mechi zao dhidi ya tukio hilo hilo.

Baada ya kufanya uamuzi wa kutoshiriki kwenye mechi hizo, wachezaji kutoka timu ya washington ya Mystics pamoja na wenzao wa WNBA, walijitosa kwenye viwanja, ili kuonyesha wazi malalamiko yao huku baadhi wakipiga goti huku wengine wakivalia t-shirt zenye maandishi ya Black Lives Matter.

Wachezaji wa timu ya Mystics walivalia t-shirts zenye jina la Jacob Blake zikiwa zimetobolewa mara 7 mgongoni kuonesha risasi aliyopigwa kijana huyo na polisi.

Shambulio la Wisconsin siku ya Jumapili limetokea miezi mitatu baada ya kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd wakati akiwa mikononi mwa polisi mjini Minneapolis, na ambalo lilisababisha maandamano makubwa kote nchini kulalamikia dhidi ya ukatili wa polisi pamoja na ubaguzi wa rangi.

Makamu wa rais Mike Pence akikubali uteuzi wake hapo jana ametowa wito wa kukomeshwa kwa ghasia mara moja, iwe ni Minneapolis, Portland au hata Kenosha.

Wakati akizungumza na wanadishi Habari Jumatano usiku, mchezaji wa timu ya Mystics Ariel Atkins alisema kuwa walichukuwa uamuzi huo baada ya kushauriana kama timu huku wakishirikisha wachezaji wengine wa WNBA.

Ariel Atkins, Mlinzi wa Washington Mystics aeleza : "Siyo kwamba sisi ni wacheza mpira wa vikapu tu, na kwa sababu sisi ni wachezaji mpira wa vikapu haimanishi hili ni jukwa letu pekee tulionalo. Inatubidi kufahamu kwamba tunapomaliza kucheza na tukienda nyumbani sisi ni watu weusi, na kwa hivyo maisha ya jamaa zetu ni ya muhimu."

Picha ya kumbukumbu ya Oct. 10, 2019, Timu ya Washington Mystics .
Picha ya kumbukumbu ya Oct. 10, 2019, Timu ya Washington Mystics .

Ligi za kitaifa za Baseball na soka zimeahirisha na pia mechi zao wakati bingwa mara mbili wa tennis upande wa wanawake Naomi Osaka ametoa taarifa akiungana na wenzake kwa kujiondoa kwenye nusu fainali ya michuano ya Western na Southern Open inayoendelea mjini New York.

Shirikisho la NBA pia limeahirisha mechi 3 za finali zilizokuwa zifanyike Jumatano baada ya timu ya Milwaukee Bucks kususia mechi yao. Timu hiyo ilijitokeza mbele ya waandishi habari na kutoa sababu zake za kutoshiriki kwenye mechi dhidi ya timu ya Orlando Magic. Forward wa timu hiyo Sterling Brown na mlinzi George Hill walizungumza kwa niaba ya wenzao.

Sterling Brown, Mchezaji wa NBA aeleza : "Miezi mitatu iliopita imetuangazia ubaguzi wa rangi ulioko dhidi ya jamii za Wamarekani Weusi. Watu kote nchini wametumia sauti zao pamoja na majukwaa tofauti kukemea uovu huo. Licha ya shinikizo hilo, hakuna hatua iliochukuliwa. Kutokana na hilo, basi sasa ni lazima tuangazie tatizo hilo kando ya mpira wa vikapu."

Hatua ya wachezaji wa NBA kususia mechi zao Jumatano imetokea siku moja tu baada ya kocha wa timu ya Los Angeles Clippers Doc Rivers kusema kuwa wamarekani wanahitaji kuongeza sauti yao kudai kutendewa vyema zaidi baada ya kupigwa risasi kwa Jacob Blake ambaye bado anatibiwa hospitalini.

Doc Rivers, Kocha wa LA Clippers asema : "Inahuzunisha sana, kwanza ninapotazama mkutano wa kitaifa wa chama cha Republikan ambapo wengi wanaozungumza wanaeneza woga. Kitu unachosikia ni Donald Trump na wote wakizungumzia hofu. Sisi ndio tunaouwawa. Sisi ndiyo tunanyimwa haki ya kuishi miongoni mwa jamii fulani."

XS
SM
MD
LG