Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 21:32

Kifo cha George Floyd : Masanamu, alama za kibaguzi vyabomolewa na waandamanaji duniani


Waandamanaji mbele ya White House wakilaani vitendo vya polisi dhidi ya George Floyd, Juni 10, 2020 Washington, DC.
Waandamanaji mbele ya White House wakilaani vitendo vya polisi dhidi ya George Floyd, Juni 10, 2020 Washington, DC.

Maandamano yameendelea kwa siku ya 16 mfululizo Jumatano ingawa waandamanaji walikuwa wachache kabisa katika miji kadhaa ya hapa Marekani huku juhudi zikiendelea kujaribu kuleta mabadiliko katika mfumo wa sheria kadamizi na polisi. 

Kwa upande mwingine watu wamekuwa wakivunja sanamu na alama zote zinazowakilisha ubaguzi wa rangi na ukoloni hapa Marekani na hata Ulaya.

Vuguvugu la maandamano limepungua sana Jumatano lakini waandamanaji wamekuwa wakibomoa, kuharibu na kuvunja vichwa vya sanamu ya Christopher Columbus kuanzia miji ya Boston upande wa kaskazini hadi Miami huko kusini. Wakati huohuo wito ukitolewa kuondolewa alama zote zinazowakilisha wakoloni na wamiliki utumwa baada ya maandamano yaliochochewa na kifo cha George Floyd wiki tatu zilizopita.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi ametaka kuondolewa kwa sanamu kubwa 11 za wanajeshi na maafisa wa enzi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe hapa Marekani mwaka 1861 hadi 1865.

Wito huo umetolewa wakati bunge lilikuwa linasikiliza pia mapendekezo ya mageuzi katika vikosi vya polisi ambapo kaka yake George Floyd, Philonise, amewarai wawakilishi kusikia kilio cha wananchi cha kuleta megeuzi.

Philonise Floyd kakake George Floyd

“Tafadhali sikilizeni wito ninaotoa hapa, wito wa familia zetu, wito unaosikika barabarani kote duniani. Watu wa tabaka zote, jinsia zote na rangi zote wameungana kuomba mageuzi,” amesema Philonise.

Juhudi za kondoa alama za ukoloni na ubaguzi zimefanyika katika nchi kadhaa za dunia. Huko Nairobi, Kenya sanamu la Malkia Victoria imebomolewa na Samuel Obiero mkazi wa mji huo anasema sanamu hizi za kikoloni zinabidi kuondolewa kote duniani.

Obiero: “Sanamu hii ina nikumbusha machungu na tabu zilizowakumba mababu zetu chini ya mikono ya wakoloni na kila mara tunapozitizama tunakumbushwa maovu yaliyoitendwa. Ndio maana tunahitaji kuziondowa kote duniani.”

Masanamu yameondolewa pia, Uholanzi Ubelgiji na Uingereza ambapo pia kuna majadiliano juu ya kuondolewa sanamu mbalimbali zinazo kumbusha enzi za ukoloni na utumwa.

Huko Palestina kwenye Ukingo wa Magharibi katika mji wa Bethlehem mchoraji asiyejulikana amechora picha kubwa ya George Floyd kwenye ukuta unaowatengenisha na Israel. Kwa Wapelstina wengi kama Hani Al-Halabi mjumbe wa chama cha vijana wa palestina, kifo cha Floyd kinawakumbusha vita vyao vya uhuru,

Hani Al-Halabi, Mwanachama wa chama cha vijana Palestina amesema : Tunatoa wito kwa taasisi za kimataifa, mashirika ya haki za binadam nan chi zote huru kutoa heshima zao kwa George Floyd na Mpalestina Iyad Hallak na kuwachukulia ni mashujaa wa kupigania uhuru na ubinadamu katika kiwango cha kimataifa.

Kwa upande wake Rais Donald Trump amepanga kukutana na viongozi wa kidini, maafisa wa Polisi na wamiliki wa biashara ndogo ndogo Alhamisi huko Dallas wakati anatafakari juu ya namna ya kujibu matakwa ya waandamanaji yaliyofuatia kifo cha George Floyd.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG