Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 07:50

Obama awasifu vijana wanaoandamana kutaka mabadiliko


Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama
Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama

Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, alisema Jumatano kuwa anaamini Marekani itakuwa bora zaidi kutokana na kuwa vijana wako kwenye mstari wa mbele kushinikiza mabadiliko kupitia maandamano yanayoendelea kushuhudiwa.

Katika hotuba yake ya kwanza tangu mwanaume Mmarekani mweusi, George Floyd kuuawa katika mazingiora yaliyoibua utata na mjadala mkubwa wa kitaifa, Rais Obama alisema kuna tofauti kubwa kati ya sasa na miaka ya 60, ambapo harakati za kutetea haki za wachache katika jamii, hazikutekelezwa na watu wa tabaka mbalimbali kama ilivyo leo.

"Nimesikia baadhi ya watu wakisema msukumo huu unaoendelea sasa unawakumbusha maiaka ya sitini. Lakini ukiangalia sasa, kuna tofauti," alisema mwanasiasa huyo.

Obama alisema hayo wakati wa mkutano kwa njia ya mtandao uliofadhiliwa na shirika la Obama Foundation.

Bila kutaja jina la yeyote, rais huyo alisema kuwa ni wakati wa kushinikiza walioko madarakani kuchukua hatua.

Obama alisema kuwa ni wakati wa kufahamu kuwa maisha na ndoto za wale wanaojihisi wanalengwa yana thamani.

"Ni wakati wa kila mmoja kutembea anakotaka bila kuwa na wasiwasi wa kushambuliwa," alisema.

Aliongeza pia kuwa jukumu kubwa liko kwa walinda sheria kwa kuwa watu wengi wamegadhabishwa na tabia za baadhi ya maafisa wa polisi.

Hata hivyo alisema kuwa polisi wengi wanatekeleza jukumu lao ipasavyo na kwamba wamekaribiswa kwenye mjadala unaoendelea.

-Imetayarishwa na Harrison Kamau, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG