Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:42

UNHCR yaiomba Tanzania kutowakatalia hifadhi wakimbizi wa Msumbiji


Cabo Delgado, Zaidi ya watu elfu moja waliosafirishwa kutoka Palma wakisubiri bandari ya Pemba baada ya kuwasili Aprili 1, 2021 baada ya kukimbia machafuko huko Palma Machi 24, 2021.(Photo by Alfredo Zuniga / AFP)
Cabo Delgado, Zaidi ya watu elfu moja waliosafirishwa kutoka Palma wakisubiri bandari ya Pemba baada ya kuwasili Aprili 1, 2021 baada ya kukimbia machafuko huko Palma Machi 24, 2021.(Photo by Alfredo Zuniga / AFP)

Shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limerudia tena wito wake kwa Tanzania kutowarudisha kwa nguvu wakimbizi wa Msumbiji wanaotafuta hifadhi, wakikimbia ghasia katika jimbo la kaskazini la msumbiji la Cabo Delgado.

Mwandishi wa VOA wa Geneva anaeleza juu ya wito uliotolewa Jumatano baada ya ujumbe wa shirika hilo pamoja na mashrika mengine kutembelea jimbo hilo.

Ripoti zinaeleza kwamba Tanzania imewarudisha zaidi ya raia wa msumbiji 4,000 waliokuwa wanaomba hifadhi tangu mwezi wa Septemba.

Shirika la kuwahudumia wakimbizi UNHCR linasema hiyo ni pamoja na watu 1,500 waliolazimishwa kurudi mwezi uliyopita.

Kwa wakati huu watu hao wanaishi katika hali ngumu ya maisha kwenye kituo cha mpakani cha Negomano upande wa msumbiji.

Msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov anasema ujumbe wa shirika hilo ulifuatana na wajumbe wa mashirika mengine ya huduma za dharura hadi eneo hilo ambalo si rahisi kufika mwezi uliyopita.

Anasema watu waliorudishwa wamewaambia wajumbe kwamba walikuwa na matumaini ya kupata hifadhi huko Tanzania baada ya kukimbia mashambulio yaliyofanywa na kundi lenye silaha kwenye mji wa Palma mwezi wa machi.

Wanasema walilazimishwa kurudi na maafisa wa serikali ya Tanzania baada ya kutembea kwa siku kadha katika eneo la msitu na mito kuweza kufika Tanzania.

Cheshirkov anasema wengi wao walichukuliwa na kusafirishwa hadi shule ya karibu na kuhojiwa na maafisa wa Tanzania wale ambao hawakuweza kutoa Ushahidi wa uraia wao wa Tanzania walirudishwa kupitia kituo cha mpakani.

Karibu watu 724,000 walilazimika kukimbia makazi yao tangu kuanza kwa ghasia kwenye jimbo lenye utajiri wa mafuta la Cabo Delgardo mwaka 2017. Mashirika ya misaada ya dharura yamekuwa hadi hivi sasa yakiwapatia msaada na hifadhi watu 50,000.

XS
SM
MD
LG