Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 29, 2022 Local time: 04:09

UN yalaani vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu Uganda


Wafuasi wa mwanasiasa Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, wakifunika nyuso zao kujikinga na bomu la machozi wakati polisi wakimkamata Kyagulanyi akifanya kampeni za urais mjini Luuka, Uganda, on Novemba 18, 2020.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres Ijumaa jioni amelaani vitendo vya ghasia vinavyoendelea nchini Uganda na kuzitaka mamlaka husika “kuhakikisha kuwa wale wote wanaoendeleza ukiukaji wa haki za binadamu wanawajibishwa.” 

Kadhalika amezitaka mamlaka hizo “kuwamwachia mara moja mtu yoyote ambaye amekamatwa kiholela.”

Guterres amewataka viongozi wa siasa na wafuasi wao “ kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa amani, na kufuata kanuni zinazohusika, na kujizuia kuchochea ghasia au kauli za chuki.”

Jeshi la Polisi nchini Uganda Ijumaa liliripoti kuwa watu wasiopungua 37 wameuawa wakati wa maandamano kufuatia kukamatwa kwa mgombea urais wa upinzani Roberty Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine siku ya Jumatano.

Mwanamuziki huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa mwenye umri wa miaka 38 aliachiwa kwa dhamana Ijumaa katika mji wa mashariki wa Iganga baada ya kufunguliwa mashtaka ya kukaidi muongozo wa COVID-19 unaotaka mikutano ya uchaguzi kuwa na watu chini ya 200.

Wine ambaye amewahi kukamatwa mara kadhaa katika miaka ya karibuni, anaonekana kuwa ni mshindani makini wa Rais Yoweri Museveni, ambaye ametawala kwa takriban miongo minne. Amerejea mara kadhaa kumtaka Museveni astaafu.

Wakati akiwa kwenye kampeni Alhamisi, Museveni amesema baadhi ya makundi ya waandamanaji yanatumiwa na watu wa nje wasiopendelea utulivu nchini Uganda. Ametishia kuwa yeyote aliyeanzisha ghasia atajuta.

Museveni anatarajiwa kulihutubia taifa siku ya Jumapili, kwa mujibu wa msemaji wake.

Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika Januari 14 nchini Uganda.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG