Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 09, 2022 Local time: 03:17

Museveni aahidi kulinda hali ya baadaye ya Uganda; Bobi Wine aendelea kupata ufuasi mkubwa


Yoweri Museveni - Rais wa Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kwamba maeneo ya Uganda ambayo yalikumbwa na vita miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, yamebadilika sana, yameshuhudia maendeleo chini ya uongozi wake. Amesema ana furahia maendeleo yamepatikana eneo la Acholi tangu alipoingia madarakani mwaka 1986.

Amesema haya katika mkutano na viongozi wa chama tawala cha National resistance movement NRM, kutoka wilaya za Lamwo, Agago, Pader na Kitgum.

Eneo la Acholi lilikumbwa na vita vibaya vilivyoongozwa na waasi wa Lords resistance movement – LRA. “Nilikuja hapa mara ya kwanza mwaka 1979 na kulikuwepo maduka machache san ana hotel moja tu ambayo ilikuwa ndogo sana, ilikuwa inaitwa Hilltop. Kwa sasa, kuna maduka mengi sana. watu wameanza kujenga nyumba zenye paa za mabati na kuachana na nyumba za nyasi. Hii ni ishara ya maendeleo,” amesema Museveni katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa michezo wa Booma, wilayani Kitgum.

Museveni, mwenye umri wa miaka 76 na ambaye anagombea muhula wa sita madarakani, amesema kwamba iwapo wagombea wengi wanazuru sehemu mbali mbali za nchi kuomba kura, hakuna yeyote kati yao mwenye ujuzi wa kuongoza nchi kumshinda.

“Tumekuja kuomba kura. Tunashindana na baadhi ya watu wanaosema kwamba wanataka kuchukua madaraka. Hakuna mwenye ujuzi kunishinda. Sehemu hii imepata amani kwa sababu ya chama cha NRM. Tulimshinda hata Kony.” Amesema Museveni

Joseph Kony ni kiongozi wa kundi la waasi la Lords’ resistance army ambalo lilianzishwa kwa lengo la kupigana vita na kumuondoa madarakani rais Yoweri Museveni.

Kundi hilo lilishindwa nguvu na kukimbilia Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Museveni amekuwa akishindwa Kitgum kwa miaka mingi

Chama tawala cha NRM kimekuwa kikishindwa katika uchaguzi mkuu wilayani Kitgum.

Kilishindwa mara nne katika ucghaguzi wa miaka ya 2001, 2006, 2011 na 2016.

Chama cha upinzani Forum for democratic change – FDC, kimekuwa kikishinda viti vingi katika uchaguzi enep la Acholi.

Wakati Museveni akiendelea na kampeni kaskazini mwa Uganda, mwanamziki na mwanasiasa Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, ambaye anaonekana kuwa mshindani wake mkuu katika uchaguzi mkuu wa Januari 2021, ameendelea kuungwa mkono na wanasiasa maarufu katika vyama vingine vya upinzani, wanaotaka wagombea wengine kumuunga mkono.

Mbunge wa Kampaka Muhammad Nsereko, ambaye ni maarufu sana katika siasa za Uganda, na ambaye alikuwa mwanachama wa chama tawala cha NRM, ametaka wagombea wengine wote wa urais kutoka vyama vingine vya upinzani, kumuunga mkono Bobi Wine, akisema kwamba kulingana na mazingira yalivyo, ndiye anayeweza kushindana na rais Museveni.

Nsereko alikuwa Akizungumza katika kipindi cha televisheni moja ya washirika wa sauti ya Amerika jijini Kampala, cha NBS TV.

“Ukweli wa mambo kwa sasa ni kwamba Robert Kyagulanyi ni wimbi la mabadiliko. Sote tukiungana na kumuunga mkono, mabadiliko yatakuja.” Amesema Nsereko.

Wanasiasa zaidi wamuunga mkono Bobi Wine

Matamshi yake Nsereko yanajiri saa chache baada ya naibu mwenyekiti wa chama cha Democratic party – DP Fred Mukasa Mbidde, kutangaza kwamba anamuunga mkono Bobi Wine, badala ya kumfanyia kampeni mwenyekiti wa chama Nobert Mao, akisema haoni mgombea mwingine wa upinzani mwenye uwezo wa kushindana na rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa Januari 2021.

Mbidde, ambaye ni wakili na mwanasiasa maarufu katika ya jamii ya Baganda, amesema kwamba mwenyekiti wake amempa ruhusa ya kumfanyia Bobi Wine Kampeni.

Mbunge maarufu kaskazini mwa Uganda Odonga Otto, naye ametangaza kwamba atamfanyia Bobi Wine kampeni, badala ya chama chake cha Forum for democratic change.

Bobi Wine afanya kampeni mashariki mwa Uganda

Bobi wine ameendelea na kampeni yake katika maeneo ya mashariki mwa Uganda, idadi kubwa ya watu wakiendelea kujitokeza barabarani na kuusindikiza msafara wake licha ya marufuku ya tume ya uchaguzi ya watu kutokusanyika kutokana na janga la virusi vya Corona.

Ujumbe wake katika kampeni unamlenga rais Museveni moja kwa moja, akidai kwamba chini ya utawala cha chama cha NRM, Uganda haina usawa katika usambasaji wa raslimali za nchi.

Ameendelea kukosoa utawala wa Museveni kwa ukandamizaji wa haki za kiraia, polisi kutumia nguvu kuzidi kiasi na kukandamiza wanaisasa wa upinzani.

Katika mikutano yake yote, Bobi Wine amekumbana na polisi ambao mara nyingi wametumia gesi ya kutoa machozi na risasi kuwatawanya wafuasi wake bila mafanikio.

Gen Mugisha Muntu ashauri jeshi kutotumiwa kisiasa

Aliyekuwa kamanda wa jeshi la Uganda Generali Mugisha Muntu, ambaye anagombea urais kwa tiketi ya chama cha Alliance for National Transformation -ANT, naye amewawataka wanajeshi kutotumiwa kisiasa kuvuruga mikutano ya kampeni ya wagombea wa upinzani.

Katika mikutano yake ya kampeni maeneo ya Masaka, Muntu amesema kwamba hakushiriki vita vilvyomuwezesha Museveni kuingia madarakani ili kufuata kila analosema wala kutenda bali kwa maslahi ya taifa.

Matamshi yanajiri siku chache baada ya mmoja wa wanajeshi wenye ushawishi mkubwa katika jeshi la Uganda, Brig. Deogratius Sunday, kusema kwamba jeshila Uganda UPDF, halipo tayari kupokeza madaraka kwa wagombea wa upinzani kwa sababu hawapo tayari kupoteza walichopigania.

Mgombea wa chama cha FDC akamatwa

Mgombea wa urais kupitia chama kikuu cha upinzani Patrick Amuriat Oboi, amekamatwa na polisi kaskazini mwa Uganda, katika wilaya ya Kitgum.

Kulingana na ratiba ya tume ya uchaguzi, Amuriat alitarajiwa kufanya kampeni katika wilaya ya Lamwo na Kitgum, jumanne, kaini polisi wamemzuilia na kumkamata kwa sababu rais Yoweri Museveni alikuwa bado anafanya kampeni sehemu hizo.

Ameachiliwa baadaye jioni baada ya Museveni kumaliza kampeni yake.

Museveni aelekea Karamoja

Rais Museveni anatarajiwa kukampeni eneo la Karamoja, ambalo katika uchaguzi uliopita alipata ushindi mkubwa kutokana na juhudi zake za kumaliza wizi wa mifugo na kunyang’anya silaha makundi ya wapiganaji.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG