Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 03:37

Bobi Wine ashtakiwa kwa 'kukiuka kanuni za Covid-19' kwenye mikutano ya kampeni


Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine.
Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine.

Polisi nchini Uganda Jumatano walimfungulia mashtaka mgombea urais  wa upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, kwa "kufanya kitendo ambacho kinaweza kusababisha kusambaa kwa virusi vya covid 19," gazeti la Serikali la New Vision limeripoti.

Mapema asubuhi, Bobi Wine alikamatwa na polisi kabla ya kuelekea kwenye kampeni yake katika wilaya ya Luuka iliyo mashariki mwa Uganda, hali ambayo ilipelekea wafuasi wake kuandamana.

Polisi wanamshtumu kwamba amekiuka masharti ya tume ya taifa ya uchaguzi, kwa kuhamasisha zaidi ya wafuasi wake 200 kuhudhuria kampeni yake, wakati tume hiyo inaruhusu watu wasiozidi 100 kushiriki kwenye kampeni za wagombea urais, ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

New vision imeripoti kuwa Bobi Wine amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Nalufenya, katika mji wa Jinja, mashariki mwa mji mkuu Kampala.

Mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Kampala, ameripoti kuwa baada ya taarifa ya kukamatwa kwa Bobi Wine, wafuasi wake wameandamana katika mji wa Masaka, kati kati mwa Uganda, na kuweka vizuizi barabarani.

Maandamano yameripotiwa pia katika mji mkuu Kampala.

Polisi wamethibitisha kwamba watu 34 wamejeruhiwa katika makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa Bobi Wine.

Tangu kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka wa 2021 kuanza, Bobi Wine amekua akizozana na polisi ambao wamemkamata mara kwa mara, wakimshtumu kukiuka maagizo ya serikali na tume ya uchaguzi ya kupambana na janga la Corona, madai ambayo anakusha.

-Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG