Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Oktoba 03, 2024 Local time: 13:18

Ukabila na Udini wahusishwa katika vita vya Sudan


Kutoka kushoto ni Jenerali Mohamed Hamdan Daglo "Hemeti" akizungumza na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan huko Khartoum tarehe 8 Oktoba 2020. Picha na Ebrahim HAMID / AFP.
Kutoka kushoto ni Jenerali Mohamed Hamdan Daglo "Hemeti" akizungumza na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan huko Khartoum tarehe 8 Oktoba 2020. Picha na Ebrahim HAMID / AFP.

Ukabila na udini unadaiwa kuhusika katika mgogoro wa kivita unaoendelea kati wa majenerali wawili wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake, Mohamed Hamdan Daglo, wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF).

Majenerali hao wanagombania madaraka na maslahi ya kiuchumi hususani umiliki wa mali asili za nchi hiyo iliyopo kaskazini mashariki mwa bara la Afrika.

Waatalamu wa masuala ya migogoro na baadhi ya wanaharakati wa muungano wa makundi ya kiraia nchini Sudan ambao hawakutaka majina yao yatajwe wakihofia usalama wao, waliambia Sauti ya Amerika kuwa mgorogoro huu ambao ulizuka ghafla takribani wiki mbili zilizopita una historia inayoonyesha kuwepo kwa misingi ya ukabila na udini.

Profesa Dan Rothbath wa shule ya utatuzi wa migogoro katika chuo kikuu cha George Mason hapa Marekani alisema kwa kawaida vipengele vya migogoro yenye misingi ya udini au ukabila huwa havihusishwi moja kwa moja kuwa ni chanzo cha mgogoro.

Naye mkurugenzi wa Kituo cha Orfalea cha Masomo ya Kimataifa kilichopo katika Chuo kikuu cha California tawi la Santa Barbara profesa Mark Juergensmayer alisema “Kijuu juu inaonekana kama ni vita kati ya RSF na SAF wakati inajulikana uasili wa RSF unatokana na wanamgambo wa Janjaweed ambao wanashukiwa walihusika katika mauaji ya kikabila huko Darfur” Alisema Mark Juergensmayer

Micheal Beer, ambaye ni mkurugenzi shirila la Non violence International lililopo Washington DC. Alisema mgogoro huo unatazamwa tofauti kulingana na eneo, na kuongeza “Ukiwa katika makao makuu Khartoum mapigano yanaonekana kuwa ni ya kati ya RSF na Jeshi la Sudan, na ukiwa eneo la Magharibi yanaonekana ni ya kati ya waafika na Wasudan wenye asili ya Kiarabu”

Wanajeshi wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) huko Khartoum tarehe 23 Aprili 2023. Picha na Rapid Support Forces/ AFP.
Wanajeshi wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) huko Khartoum tarehe 23 Aprili 2023. Picha na Rapid Support Forces/ AFP.

Akielezea uasili wa mikoa wanakotoka wanajeshi wa makundi hayo yanayohasiana, Mubaraka El Amin mkazi wa jiji la Seattlle huko Washington alisema kuwa wanajeshi wengi wa wa RSF wanatoka eneo la magharibi lenye mchanganyiko wa makabila ya Afrika Magharibi kama vile Niger, Mali na Chad wakati wanajeshi wa Sudan wanatoka eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo, jeshi ambalo pia lina mahusiano na viongozi wa ngazi za juu wa utawala wa uliopita walioondolewa madarakani mwaka 2019.

"Bashir ni mlezi (Godfather) wa majenerali wote wa jeshi," alisema mwanaharakati wa kisiasa kutoka muungano wa mashirika ya kiraia ya Khartoum, na kuongeza kuwa dini inatumiwa na wanachama wa Muslim Brotherhood katika jeshi kupata uhalali wa kisiasa.

Wiki iliyopita maafisa wakuu na wa ngazi za chini wa uliokuwa utawala wa Bashir walitoroka gerezani, wakiwemo wale waliokuwa wanatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Wakati huo huo mamia ya watu wameuawa na maelfu kujeruhiwa. Umoja wa Mataifa unaripoti kuwa zaidi ya watu 430,000 wameyakimbia makazi yao. Majenerali hao wawili "wamekubaliana kimsingi kusitisha mapigano kwa siku saba kuanzia Mei 4 hadi 11," wizara ya mambo ya nje mjini Juba, Sudan Kusini ilisema katika taarifa.

-Imetayarishwa na Mariam Mniga, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG