Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 05, 2024 Local time: 01:13

Hospitali Khartoum zaelemewa na majeruhi



Wanajeshi wakimbeba kwenye gari la wagonjwa raia wa Ugiriki aliyejeruhiwa mguu baada ya kuhamishwa kutoka Sudan, tarehe 25 Aprili 2023. Picha na Aris Messinis / AFP.
Wanajeshi wakimbeba kwenye gari la wagonjwa raia wa Ugiriki aliyejeruhiwa mguu baada ya kuhamishwa kutoka Sudan, tarehe 25 Aprili 2023. Picha na Aris Messinis / AFP.

Hospitali mjini Khartoum nchini Sudan zimeelemewa na majeruhi kutokana na mapigano kati ya jeshi la Sudan na Rapid Suport Forces (RSF) yaliyoanza wiki iliyopita na kusababisha vifo vya mamia ya watu huku maelfu wakiukimbia mji huo.

Akizungumza na sauti ya Amerika kwa njia ya simu kutoka Khartoum, rais wa chama cha madaktari nchini Sudan Hiba Omar amesema, hospitali zimeelemewa na idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa huku kukiwa na upungufu mkubwa wa madaktari, wahudumu, dawa na vifaa.

Daktari Omar ambaye amekuwa akiishi katika hospitali tofauti tangu vita vilipozuka, hali ambayo imesababisha baadhi ya hospitali kufungwa na wagonjwa kuhamishwa katika hospitali nyingine hali kadhalika madaktari nao wanatoka hospitali moja hadi nyingine. Daktari huyo amesema “hali ni mbaya sana, sijalala siku ya pili leo, majeruhi ni wengi na tuna uhaba wa wafanyakazi.”

Hata hivyo Dk. Omar amesema wamekuwa wakipokea msaada wa vifaa kutoka wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF).

Mapigano makali katika mji huo Khartoum yalisababisha ugumu kwa watu kufikia huduma za msingi wakati hospitali zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi, madaktari, umeme, mafuta na “kila kitu kasoro waathirika” alisema.

Licha ya mapigano ya hapa na pale, Marekani imeweza kusimamia sitisho la mapigano la saa 72 kati ya majenerali wawili waliohasimiana, huku wakazi wa mji huo wanatumia hali ya utulivu uliopo kukusanya tena mahitaji muhimu au kuondoka mjini Khartoum.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken Jumatatu alitangaza kwamba pande zinazo zozana nchini Sudan zimekubaliana kusitisha mapigano kwa saa 72.

-Imetayarishwa na Mariam Mniga, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG