Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Oktoba 08, 2024 Local time: 21:01

Maiti zimezagaa kila kona ya Khartoum - Mashahidi


Wakazi wa Khartoum wakivikimbia vitongoji vyao tarehe 19, Aprili 2023, baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Picha na AFP.
Wakazi wa Khartoum wakivikimbia vitongoji vyao tarehe 19, Aprili 2023, baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Picha na AFP.

Mitaa ya mji mkuu wa Sudan Khartoum imejaa miili ya watu waliouawa katika mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) huku maiti hizo zikitoa harufu mbaya.

Wakaazi wa Khartoum wanaendelea kuukimbia mji huo uliogeuzwa kuwa uwanja wa mapambano. Juhudi mpya za diplomasia nazo zimegonga mwamba.

Amira Ewies, mwanasheria na mwanaharakazi anayetetea haki za binadamu nchini Sudani amesema “tunakumbana na janga la kimazingira kutokana na uwepo wa maiti zilizozagaa mitaani, baadhi zimeoza na kutoa harufu mbaya isiyo kifani”.

Ewies anasema familia zenye uwezo zimefanikiwa kuondoka mjini humo kwenda kutafuta hifadhi salama katika maeneo mengine ya nchini Sudan.

Naye Mahamood Bushala amesema wakati alipoondoka Khartoum mara tu baada ya vita kuzuka, alishuhudia maiti za watu zikiwa zimesambaa mitaani “maiti zilikuwepo kila mahali, hivi ninavyoongea marafiki zangu walioko Khartoum wanasema maiti zimekuwa nyingi, zimezagaa kila kona na zinaongezeka kila siku” alisema.

Hata baada ya kutambuliwa kwa baadhi ya maiti hizo, bado kuna ugumu kwa jamaa kuweza kuwachukua ndugu zao kutokana na hali ya mapigano yanayoendelea. Kama vile maiti ya Mohammed Slah, mwanafunzi aliyekuwa akisomea udaktari katika chuo kikuu kilichopo mjini Khartoum, maiti yake ilitambuliwa siku ya Jumatano, siku tano baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha.

“Ni huzuni kubwa maiti yake imekuwa barabarani kwa siku tano, tumeshindwa kuichukua na kuizika” mwalimu wake Dk. Ahmed Eltayeb Ibrahim aliiambia Sauti ya Amerika kwa njia ya simu kutoka Sudan.

Dk. Ibrahim ambaye pia aliweza kutoroka mjini humo siku ya Jumatano baada ya wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya chuo hicho kuhamishiwa katika hospitali zilizopo nje ya mji huo uliokumbwa na mashambulizi makali hususan katika maeneo ya uwanja ya ndege, hospitali na maeneo yaliyoko katikati ya mji ambao umejaa wanajeshi kila kona.

Dk. Ibrahim na familia yake wamekimbilia katika jimbo la Gezira, lakini nyumba yake imeharibiwa na gari lake kupigwa risasi, amesema. “Sasa niko umbali wa kilometa 200 kutoka Khartoum na familia yangu, hakuna mapigano hapa, ni salama sana, ni kijiji kidogo katika jimbo la Gezira.

Mapambano hayo ya ghafla yaliyosababisha kusitishwa kwa safari za ndege na kuwafanya baadhi wa wakaazi wa mji huo kushindwa kuondoka kutafuta hifadhi salama nje ya mji wa Khartoum.

-Imetayarishwa na Mariam Mniga, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG