Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Aprili 20, 2025 Local time: 23:16

Serikali ya Uganda kuwaadhibu wanaosaidia watoto ombaomba


Watoto wa mitaani wakiomba nchini Uganda barabarani mjini Kampala, Julai 17, 2014.
Watoto wa mitaani wakiomba nchini Uganda barabarani mjini Kampala, Julai 17, 2014.

Serikali ya Uganda imetangaza imeanza kutekeleza sheria inayopiga marufuku utoaji wa msaada wa pesa au chakula kwa watoto omba omba mitaani nchini humo, lengo kubwa likiwa ni kuwaondoa watoto hao barabarani.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu yeyote anayetoa msaada wa pesa au chakula kwa watoto omba omba, anafanya tendo la uhalifu na anaweza kufungwa miezi sita gerezani au kutozwa faini ya wastani ya shilingi 41,350.

Waziri msaidizi wa vijana na watoto Nakiwala Kiyingi, amesema wizara hiyo kwa ushirikiano wa maafisa wa usalama, wameanza kutekeleza sheria iliyopitishwa na mamlaka ya jiji la Kampala KCCA, mwezi uliopita.

Kosa la kusaidia watoto ombaomba wengi wanaliona kama ni kitendo cha ukarimu, amesema Kiyingi.

Waziri ameeleza kuwa tayari amepatiwa shilingi bilioni 3.4 kuwapa makazi na chakula watoto hao ombaomba barabarani.

“Hakuna tena kumpa mtoto ombaomba pesa au hata ndizi. Ukifanya hivyo ni sawa na kuchangia kufanya kosa la uhalifu. Hawa watoto wanatumika kama biashara. Wanaomba kwa niaba ya watu wazima,” amesema.

“Kwa kila kundi la watoto watano, kuna mtu mzima hapo karibu amejificha kukusanya pesa unazowapa hawa watoto. Tunajua mambo haya yote. Kwa hivyo, usitoe msaada wa chakula wala pesa kwa watoto walio barabarani, ni jukumu langu kufanikisha mahitaji yao kwa sababu nimepewa pesa na serikali,” amefafanua waziri Kiyingi

Lakini Younous Lubuuka, mhadhiri wa masuala ya kijamii Chuo Kikuu cha Kyambogo, ambaye pia ni mtetezi wa haki za kiraia, anasema matumaini ya hatua ya serikali kufaulu ni madogo.

“Yana nia njema. Wale wanaoweza kuwaweka shuleni, wawaweke shuleni. Wakupewa mafunzo ya kazi ya kimaisha waweze kujitegemea, nao wapewe. Ni sera nzuri, ni sheria nzuri lakini utekelezaji wake ndio tatizo. Naona ni jambo ambalo halitafaulu”, amesema Lubuuka

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Watoto na Vijana ya Uganda, jumla ya watoto 15,000 wanapatikana kwenye barabara za Uganda, wakitegemea ukarimu wa wapita njia kuwalisha, 2000 kati yao wakiwa jijini Kampala.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Kennes Bwire, Washington, DC

XS
SM
MD
LG