Hiyo ni baada ya kusikika milio ya bunduki kwenye kambi mbali mbali za kijeshi na kusababisha kuwepo na ripoti kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna mapinduzi nchini humo.
Akizungumza kwenye televisheni ya taifa Jenerali Simpore, amesema kwamba kumekuwepo na matukio kadhaa katika baadhi ya kambi na kwamba wanafanya uchunguzi.
Wakazi wa mji mkuu wa Ouagadougou wanasema milio ya bunduki ilianza kusikika tangu jana usiku kwenye kambi ya Sangoule Lamizana na jeli za kijeshi.
Wanajeshi wanasemekana wamefanya uasi huo ili kutaka wakuu wa majeshi ya Burkina Faso wajiuzulu na kudai kupatiwa silaha na vifaa vinavyostahiki ili kupambana na wanamgambo wa Kiislamu kaskazini mwa nchi.
Malalamiko hayo yanatokea siku 12 baada ya kukamatwa watu 12 akiwemo afisa wa cheo cha juu wa jeshi kwa dhana ya kupanga mapinduzi katika nchi ambayo imekumbwa na miaka saba ya uasi unaofanywa na wanamgambo wa Kiislamu.
Wakati huo huo polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mamia ya watu waliojitokeza kwenye uwanja mkuu wa Ouagadougou ili kuunga mkono uasi unaofanywa na wanajeshi.
Waandamanaji hao wamekuwa pia wakitoa wito kwa Rais Roc Marc Kabore kuachia madaraka kwa kushindwa kukabiliana na mashambulio ya wanamgambo.
Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali