Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 07:31

Samia ahimiza mahusiano thabiti ya kimataifa kukabiliana na COVID-19


Rais Samia Suluhu Hassan
Rais Samia Suluhu Hassan

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa ushirikiano na ubinadamu visikubali kabisa kuemewa na virusi vya corona.

Akizungumza katika Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Alhamisi, mjini New York, Rais Samia ameeleza kuwa anaunga mkono maudhui ya mkutano huu unaohimiza kujenga nguvu ya kujizatiti kwa kuwa na matumaini ya kutokomeza COVID-19, kujenga uwezo endelevu, kukabiliana na mahitaji ya dunia, kuheshimu uhai wa watu, na kuimarisha taasisi ya Umoja wa Mataifa.

Rais aliongeza : “Siyo kwa bahati nasibu nimechagua kuhudhuria mkutano huu wa UNGA ikiwa ni safari yangu ya kwanza nje ya Afrika tangu niwe Rais. Nimefanya hivi kwa hisia zangu za dhati za kuwa ni muumini na mkereketwa wa kujenga mahusiano ya kimataifa katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia yetu hivi leo.”

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Rais Samia pia ameihakikishia dunia kuwa chini ya usimamizi wake, Tanzania itaendelea kuwa mwanachama hai wa UN, mshirika wa kutegemewa katika ushirikiano wa kimataifa na “tutaendelea kukunjua mikono yetu kwa wote watakaotaka kutupokea na kushirikiana nasi.”

Kuhusu suala la janga la COVID-19 na upatikanaji wa chanjo ya kuzuia ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, Rais wa Tanzania alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu na wadau katika kufanya juhudi za kutokomeza ugonjwa huu.

“Wakati dozi za chanjo zimetolewa kwenye nchi zenye kipato cha juu na cha kati, kwa hali ilivyo hivi sasa sio rahisi kuwa tutafikia lengo la WHO la kuwachanja angalau asilimia 40 ya watu katika kila nchi ifikapo mwisho wa 2021. Na angalau asilimia 70 ifikapo nusu ya mwaka 2022,” Rais amesema.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus

Rais ametahadharisha kuwa : “ni vyema nchi zilizokuwa na chanjo za ziada kutoa kwa nchi nyingine. Hasa ukizingatia kuwa nchi hizo tayari zimeanza kuwapatia watu wake chanjo ya tatu maarufu kama ‘Booster.” Tunajisahau kuwa hakuna mtu aliye salama mpaka watu wote wawe wako salama.”

Rais Samia ameomba haki miliki ya chanjo ya COVID-19 iondoshwe kwa nchi zinazoendelea ili waweze kumudu kuzalisha chanjo. Hii siyo tu hatua muhimu kumaliza janga hili, lakini ni jambo sahihi kufanyika kuokoa wanadamu.

Kuhusu hali ya uchumi amesema Tanzania kama nchi nyingine haikuachwa na athari za janga hili. Kabla ya COVID-19 uchumi wa nchi ulikuwa unakua kwa kiwango cha asilimia 6.9 ukilinganisha na ukuaji wa hivi sasa ambao unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.4.

Samia amesema changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa zimeathiri vibaya sana maisha ya watu, amani na usalama wao na kuwalazimisha kukimbia makazi yao.

Amesema Tanzania inatumia asilimia tatu ya pato lake la taifa kukabiliana na athari hizo na kujenga uimara wake. “Hali hii ni mzigo mzito kwa nchi ambayo inapambana na umaskini uliochanganyika hivi sasa na kuzuka kwa janga la COVID-19. Janga hili limedhoofisha uwezo wetu wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yenye athari za muda mrefu,” amesisitiza.

Pia ametoa wito wa kuwepo uwazi katika taratibu za kugawa fedha kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa na kusisitiza kuwa nchi zilizoendelea zitekeleze ahadi zao kwa kuchangia dola za Marekani 100 bilioni kila mwaka hadi ifikapo 2025 ili kuwezesha utekelezaji wa makubaliano yaliofikiwa Paris.

Samia aeleza kipaumbele cha Tanzania katika mkutano wa UN
please wait

No media source currently available

0:00 0:03:29 0:00

Rais Samia pia ameeleza kuwa wakati ikiwa tumebakisha chini ya muongo mmoja mbele yetu, kufikia malengo yetu ya SDGs ifikapo 2030, ripoti ya 2020 inaonyesha dunia haiendi sambamba na ajenda ya kufanikisha malengo ya 2030 kutokana na athari hasi za COVID-19.

“Hali hii itarejesha nyuma maendeleo yaliyofikiwa miaka ya nyuma takriban watu 70 waliotoka katika umaskini watatumbukia huko tena kwa sababu ya janga la corona.”

“Kwa kweli kinachosikitisha ni kuwa athari hizi haziko sawa kote duniani. Sisi katika nchi zinazoendelea ndio tunaoathirika zaidi. Na hivyo basi ni lazima kuwe na juhudi za pamoja kutatua hali hii yenye maangamizi,” amesema.

Rais amezishukuru taasisi za kimataifa kwa juhudi zao kuzisaidia nchi kuondoka katika hali mbaya ya uchumi, na hivyo hatua hizi zilizochukuliwa ni muhimu sana.

Tanzania kama nchi nyingine imeathiriwa na COVId-19 na tulichukua hatua zilizopendekezwa na Shirika la Afya Duniani kwa ajili ya kuokoa maisha, Rais Samia ameeleza.

“Lakini kutokana na sehemu kubwa ya watu nchini kuishi kwa uchumi wa kujikimu ambao tunahitaji kuwasaidia waendelee kuishi, nchi yangu ilifuata hatua zote muhimu kuzuia kuenea kwa COVID-19,” alifafanua.

Alieleza kuwa Kampeni ya chanjo ilianza tangu mwezi Julai mwaka 2021 kwa kuwachanja wale walio katika hatari zaidi. “Pia tumejiunga na Utaratibu wa kupatiwa chanjo ya COVID-19 unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa,”Rais alieleza.

Katika hotuba yake ya kwanza kama Rais wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Rais Samia amewashukuru nchi wanachama wa UN kwa niaba ya taifa lake kwa ujumbe wa rambi rambi waliotuma kufuatia kufariki kwa hayati rais John Pombe Magufuli.

Gari Maalumu la Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ likiwa limebeba Jeneza lenye Mwili wa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati likiwasili katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma kwa aj
Gari Maalumu la Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ likiwa limebeba Jeneza lenye Mwili wa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati likiwasili katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma kwa aj

Amesema ujumbe huo ulileta utulivu kwa taifa na “kutuwezesha kukabiliana na hali ya majaribio iliyokuwa haijawahi kutokea kwa taifa letu.”

“Pia tunatoa shukurani zetu kwa rais wa UNGA aliyemaliza muda wake kwa kuipa fursa Tanzania katika mkutano wa Baraza Kuu wa mwezi Aprili kutoa rambirambi kwa rais wetu mpendwa aliyeaga dunia. Kwa hakika hii ilikuwa ishara ya udugu na umoja,” alisema.

XS
SM
MD
LG