Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 08:34

Rais wa zamani wa Ivory Coast atarajiwa kuwasili nyumbani


Laurent Gbagbo
Laurent Gbagbo

Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, anatarajiwa kurejea nchini Alhamisi kwa mara ya kwanza tangu alipokamatwa na kukabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, mnamo mwezi Novemba mwaka 2011.

Kiongozi huyo alikuwa anakabiliwa na tuhuma za kuhusika katika mgogoro wa baada ya uchaguzi uliotokea kati ya mwaka 2010 na 2011.

Gba-gbo alipatikana bila hatia kwa mashtaka yote tarehe Januari 15, 2019, na ICC ilithibitisha kuachiliwa kwake, mwezi Machi mwaka 2021.

Mamlaka nchini Ivory Coast, zimeahidi kwamba atapokelewa kwa heshima zote za kiongozi wa zamani wa nchi, na hata Rais wa nchi hiyo kutangaza kwamba serikali itagharamia nauli yake ya ndege.

Kurejea kwa Gba-gbo kunatarajiwa kukiongezea nguvu chama chake cha Ivorian Popular Front ambacho kimekumbwa na mgawanyiko kwa miaka kadhaa sasa.

Mipango yake ya kisiasa haieleweki, lakini wachambuzi wanasema huenda akachukua jukumu muhimu kama kiongozi wa upinzani.

Kiongozi huyo wa zamani bado anakabiliwa na mashtaka mengine ndani ya nchi ambako alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani mwaka 2018, akiwa pamoja na wengine, ambao baadaye walisamehewa na Rais Alasane Ouatarra.

Vyanzo vya habari : AFP/Reuters

XS
SM
MD
LG