Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 04:51

Kura zahesabiwa Guinea, ghasia  zaripotiwa Ivory Coast 


Wananchi wakiwa wamepanga msitari kupiga kura Conakry, Guinea, Jumapili, Oktoba 18, 2020. (AP)
Wananchi wakiwa wamepanga msitari kupiga kura Conakry, Guinea, Jumapili, Oktoba 18, 2020. (AP)

Nchini Ivory Coast, watu wawili wamefariki katika ghasia za uchaguzi, ikiwa ni wiki mbili kabla ya upigaji kura katika uchaguzi mkuu kwenye nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Kura zinaendelea kuhesabiwa nchini Guinea, baada ya uchaguzi mkuu wa jana jumapili, huku rais wa sasa Alpha Conde, mwenye umri wa miaka 82 akitarajiwa kushinda muhula wa tatu madarakani.

Polisi wameimarisha usalama kote nchini Guinea baada ya kutokea ghasia katika sehemu tofauti za nchi, kupinga hatua ya Conde kuwania muhula wa tatu.

Polisi wamesema kwamba shughuli ya kupiga kura ilifanyika katika mazingira yenye utulivu.

Uchaguzi huo umefanyika baada ya miezi kadhaa ya maandamano yaliyopelekea watu kadhaa kuuawa katika msako wa maafisa wa usalama dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakimpinga rais Alpha Conde.

Conde anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kiongozi wa upinzani Cello Diallo na wagombea wengine 10. Tayari Diallo amedai kwamba huenda rais Conde akafanya udangayifu katika hesabu ya kura.

Kumekuwepo wasiwasi kwamba machafuko ya hivi karibuni yamechukua mkondo wa kikabila, rais Conde akishutumiwa kwa kusababisha migawanyiko kwa manufaa yake ya kisiasa, shutuma ambazo amekana.

Siasa za Guinea hugubikwa sana na ukabila. Rais Conde anatoka jamii ya Malinke huku mpinzani wake - Diallo, akitoka jamii ya Fulani.

Kuna wasiwasi mkubwa nchini Guinea kwamba huenda kukatokea ghasia baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi ambayo yatachukua mda kutolewa.

Ghasia katika kampeni Ivory coast

Nchini Ivory Coast, watu wawili wamefariki katika ghasia za uchaguzi, ikiwa ni wiki mbili kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu wa urais katika nchi hiyo ya Afrika magharibi.

Ghasia hizo zilianza ijumaa katika mji wa Bongouanou, ambayo ni ngome ya mgombea wa upinzani Pascal Affi N'Guessan, kilomita 200 kutoka mji wa kibiashara wa Abidjan.

Mfanyabiashara kutoka kabila la Agni, anayetambuliwa kuwa mfuasi wa upinzani, alipigwa risasi na kuuawa.

Kulingana na walioshuhudia ghasia hizo, mtu mmoja kutoka kwa kundi linalodaiwa kuwa linaunga mkono serikali, ameuawa.

Kulingana na shirika la habari la AFP, maduka mengi na migahawa katika mji wa Bongouanou, imechomwa moto na magari kadhaa kuharibiwa.

Karibu watu 15 waliuawa katika makabiliano ya kijamii mnamo mwezi Agosti na Septemba, katika miji kadhaa nchini Ivory Coast, baada ya rais Alassane Outtara kutangaza nia ya kugombea mhula wa tatu madarakani.

Watu 3,000 waliuawa katika machafuko ya mwaka 2010 yaliyoendelea hadi mwaka 2011 nchini Ivory Coast.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG