Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 15, 2024 Local time: 06:15

Polisi Uganda yachunguza tukio la wanajeshi kuvamia kituo cha polisi


Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Polisi nchini Uganda wanachunguza tukio ambalo wanajeshi walivamia kituo cha polisi cha Ndejje, Wilaya ya Wakiso, nje kidogo ya mji mkuu Kampala Jumatano usiku.

Wanajeshi hao waliwatishia maafisa wa polisi kwa bunduki kabla ya kuwaachilia wanajeshi wenzao ambao walikamatwa kwa tuhuma za kuweka vizuizi barabarani kinyume cha sheria.

Tukio hilo lilitokea katika kituo cha Polisi cha Limuli huko Parokia ya Ndejje katika barabara ya Entebbe, Wilaya ya Wakiso.

“Tunachunguza kuongezeka vitendo vya ujambazi na pia kuwasaidia watuhumiwa kutoroka kutoka katika ulinzi wa polisi,” naibu msemaji wa polisi mjini Kampala, Luke Owoyesigyire alisema Alhamisi.

Inadaiwa kuwa washukiwa hao waliokuwa na silaha na waliovalia nguo za kijeshi waliweka vizuizi kinyume cha sheria katika katika kijiji cha Kakoola huko Ndejje Jumatano majira ya saa tatu na nusu usiku saa za Afrika Mashariki.

Polisi yapeleka askari wa doria

Waathirika waliripoti polisi ambao walipeleka gari la doria likiwa na maaskari wenye silaha.

Mara baada ya kuliona gari la polisi, washukiwa hao walipiga risasi hewani. Lakini maafisa hao walijizatiti na kukabiliana na washukiwa hao na kuwanyang’anya silaha.

Chanzo cha habari kilisema washukiwa hao, waliotambuliwa kama wanajeshi Job Reti na Orete Were, walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo cha polisi cha Limuli kwa ajili ya kuhojiwa.

Kile kilichoonekana kuwa ni mafanikio kwa polisi, hata hivyo hayakudumu muda mrefu, saa kadhaa baadaye gari aina ya Toyota Land Cruiser ikiwa na wanajeshi wanane wenye silaha lilivamia kituo hicho cha polisi. Waliwalazimisha polisi wawakabidhi washukiwa hao wawili.

Chanzo hicho cha habari pia kilisema polisi walipokataa, wanajeshi hao walitoa silaha na kuwadhibiti maafisa wa polisi na kisha kuwaachia huru washukiwa hao wawili.

Viongozi walivamia kituo cha polisi

Polisi wamewataja viongozi wa kundi hilo lililovamia kituo cha polisi kuwasaidia washukiwa hao kutoroka ni Sajenti Tonny Opio wa Jeshi la Ulinzi la Uganda na mwingine ni Pius Lutaya.

Wanajeshi hao baadae walikwenda kuripoti kituo cha polisi cha Mutungo katika wilaya ya Wakiso wakidai kuwa washukiwa hao walikuwa wamejeruhiwa na waliwachukua kutoka kituo cha polisi kwa ajili ya kuwapelekea kupata matibabu, hospitali ambayo hawakuitaja.

Kumekuwa na ongezeko la matukio ya vizuizi vya barabarani kinyume cha sheria mjini Kampala na wilaya za Wakiso, Mityana na Greater Luweero.

Wanachama wa magenge wanaoshukiwa kufanya vitendo hivyo wanaelezewa kuvaa nguo za kijeshi, kuweka vizuizi katikati ya barabara na kujifanya wako katika kuimarisha ulinzi katika maeneo wanayoweka vizuizi.

Chanzo cha habari hii kinatokana na gazeti la The East African linalochapishwa Kenya

XS
SM
MD
LG