Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 23, 2024 Local time: 19:40

Poland inatafakari kupeleka vifaru Ukraine hata bila ya idhini ya Ujerumani


FILE - Picha hii iliyopigwa May 20, 2019 yaonyesha kifaru aina ya Leopard 2 vinavyotumiwa na jeshi la Ujerumani na kutengenezwa nchini humo.
FILE - Picha hii iliyopigwa May 20, 2019 yaonyesha kifaru aina ya Leopard 2 vinavyotumiwa na jeshi la Ujerumani na kutengenezwa nchini humo.

Waziri mkuu wa Poland alisema Jumatatu kuwa nchi yake inajenga mshikamano wa mataifa  tayari kupeleka vifaru aina ya Leopard 2 vilivyotengenezwa Ujerumani huko Ukraine hata kama Ujerumani haitatoa ruhusa rasmi kupelekwa vifaru hivyo.

Mateusz Morawiecki amewaambia waandishi wa habari kwamba Poland itaomba kibali kutoka Ujerumani, lakini hilo la kuomba idhini ya Berlin siyo suala muhimu la msingi.

“Tunaendelea kuishinikiza serikali huko Berlin kuhakikisha vifaru vya Leopard vinapatikana,” Morawiecki alisema.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amekiambaikituo cha televisheni ya Ufaransa LCI Jumapili kwamba kama Poland itatakiwa kuomba kibali kupeleka vifaru aina ya Leopard 2 Ukraine, “Hatutakuwa pingamizi kwao.”

Hadi Baerbock alipotoa maoni yake, Ujerumani ilikuwa inasita kupeleka vifaru vya Leopard 2 kwa Ukraine au kuidhinisha kupelekwa na nchi ambazo zilinunua kutoka Ujerumani.

Ukraine kwa muda mrefu imekuwa ikitaka vifaru hivyo venye nguvu ili kupambana na majeshi ya Russia kwa kutumia vifaru vya kisasa zaidi ya vile ambavyo Ukraine inavitumia.

Mkuu wa wafanyakazi wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, Andriy Yermak aliandika Jumatatu kupitia ujumbe wa Telegram kuwa kile ambacho Ukraine inakitaka siyo vifaru 10-20, “ lakini ni mamia” ili kufikia lengo lake.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Jumatatu kuwa mjadala kati ya nchi za Ulaya iwapo wapeleke vifaru kwa Ukraine umeonyesha “wasi wasi unaongezeka” ndani ya NATO. Pia alionya kuwa nchi zitakazo peleka silaha Ukraine “watabeba jukumu kwa kufanya hivyo.”

Chansela wa Ujerumani Olaf Scholz Jumapili hakusema iwapo Ujerumani itawakubali kuipa Ukraine vifaru vya kivita, lakini shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa alisema maamuzi kama hayo yatafanyika kwa kushirikiana na washirika ikiwemo Marekani.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema hafuti uwezekano wa kupeleka vifaru aina ya Leclerc huko Ukraine. Alitahadharisha, hata hivyo, kupeleka vifaru isiwe sababu ya kuhatarisha usalama wa Ufaransa au kuchochea vita kati ya Ukraine na Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alisema Jumapili katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Sky News angependa kuona waukraine “wanapewa silaha kama vile Leopard 2.”

Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Michael McCaul, ambaye ameteuliwa mwenyekiti mpya wa Republikan katika Kamati ya Mambo ya Nje, amekiambia kipindi cha “This Week” cha kituo cha televisheni cha ABC kuwa Marekani ipeleke vifaru vyake vyenye nguvu aina ya Abrams huko Ukraine ili kuishawishi Ujerumani pia kupeleka vifaru vyake vya Leopard 2.

“Kifaru kimoja tu cha Abrams kitatosheleza kushawishi washirika, hasa Ujerumani, kufungua akiba yao ya vifaru kwa ajili ya vita dhidi ya Russia,” alisema.

Seneta Mdemokrat Chris Coons pia alikiambia kituo cha televisheni cha ABC kuwa wakati umefika kuweka pembeni wasiwasi wa Marekani kuhusu kupeleka vifaru vya Abrams.

“Naheshimu kwamba viongozi wetu wa kijeshi wanaofikiria Abrams ni vifaru vya kisasa, ni ghali kutumika katika vita kwa kuwa na manufaa kama vile vya Leopard, lakini tunatakiwa kuendelea kushirikiana na washirika wetu wa karibu na kusonga mbele hatua kwa hatua.

Baadhi ya taarifa hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters

XS
SM
MD
LG