Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 10, 2022 Local time: 05:22

Kenya : Moi azikwa kitaifa


Wanajeshi wa Kenya wakibeba jeneza la Rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi likiwa limefunikwa na bendera ya Kenya, katika heshima ya maziko ya kiserikali katika uwanja wa Nyayo mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Feb. 11, 2020.

Rais Mstaafu wa Kenya Daniel Arap Moi hatimaye amezikwa nyumbani kwake Kabarak katika jimbo la Nakuru katika hafla ya kitaifa iliyoongozwa na kikosi cha jeshi.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo wakiongozwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, wamewataka Wakenya kuiga hulka zake Moi za kulitaka taifa kuwa na umoja na amani ili kuyafikia malengo yake ya maendeleo.

Kwa mujibu wa itikadi na utamaduni wa jeshi la Kenya, rais huyo mstaafu alizikwa katika hafla ya kipekee kwa kupokea heshima ya kufyatuliwa mizinga 19 hewani ikiwa ni heshima ya kutumikia kwake nafasi ya urais wa Kenya, wakati huo akiwa ndiye amiri jeshi mkuu, huku wimbo wa taifa ukichezwa Ndege za kivita zikipita angani, haya yote yakiwa ni kiashiria cha heshima kwa Rais huyo mstaafu wa Kenya.

Ulinzi uliimarishwa katika eneo la kaburi lake, wanajeshi waliovalia sare rasmi za kijeshi, nyeupe na nyekundu, kando kando yao ikiwa ni familia yake, huku katika mstari wa mbele akiwa ni Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Waombolezaji wengine, kufuatia desturi za kiafrika, walivalia mavazi meusi, kipande cha kitambaa cheupe kikining’inia kwenye nguo kuashiria kuwa ulikuwa wakati wa kuomboleza.

Jeneza la kiongozi huyo wa Kenya aliyedumu kwa kipindi cha miaka ishirini na minne madarakani, lilisafirishwa kwenye gari maalum la kijeshi kutoka hifadhi ya Lee hadi uwanja wa ndege wa Wilson jijini Nairobi, na kupakiwa kwenye ndege ya kijeshi hadi nyumbani kwake Kabarak kwa hafla ya mazishi, Jumatano.

Katika hafla hiyo iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, viongozi mbalimbali walimtaja Moi kama kiongozi shupavu aliyeonyesha mengi ya kuigwa, vitendo vya kukumbatiwa wakati akiwa rais wa pili wa Kenya.

Rais Kenyatta alimtaja Moi kuwa mwalimu wake wa siasa, siasa zilizomwezesha kupata nafasi ya kuchaguliwa kuwa rais wa Kenya.

Kenyatta akiwahutubia waombolezaji wengine wengi ambao walikuwa wamevalia mashati na kofia zilizo na nembo ya chama tawala wakati huo KANU, aliwarai viongozi wa Kenya kuipenda nchi yao, kuitetea na kuilinda vilivyo.

Naye Naibu Rais wa Kenya, William Ruto aliyanukuu maneno ya Rais huyo mstaafu na kuwataka raia wa Kenya kuyaiga na kuyafanyia vitendo.

Kwa upande wake Kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga, kando na kukariri kuwa Moi alitoka katika familia ya umasikini na kuwa rais, amewataka Wakenya kufahamu kuwa unaweza kuwa rais bila kutoka katika familia ya kitajiri. Aidha, alieleza kuwa Moi alimfunza mengi yaliomsaidia.

Odinga alisema : "Familia ya Moi ilimtaja kuwa mtu aliyekuwa mhimili mkubwa, mkarimu, mcha Mungu na mpenda amani. Lakini siasa hazikuachwa nyuma.

Wazee kutoka jamii ya Kikalenjin pamoja na familia nzima ya Rais Mstaafu Moi ilimteua na kumpongeza fimbo ya nyayo ambayo ni rungu aliyotumia Moi kwa Mwanawe Gideon Moi kama ishara ya kumrithi katika siasa za chama chake.

Moi alifariki Jumanne, Februari 4, mwaka huu katika hospitali yaNairobi, huku kifo chake kikitangazwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG