Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 01:01

Aliyekuwa rais wa Kenya Daniel Arap Moi afariki


Aliyekuwa rais wa Kenya Daniel Toroitich Arap Moi aliyeaga dunia tarehe 4 mwezi Februari 2020.
Aliyekuwa rais wa Kenya Daniel Toroitich Arap Moi aliyeaga dunia tarehe 4 mwezi Februari 2020.

Aliyekuwa rais wa Kenya Daniel Toroitich Arap Moi aliaga dunia Jumanne asubuhi akiwa na umri wa miaka 95.

Moi aliliongoza taifa hilo la Afrika mashariki kwa miaka 24 tangu mwaka wa 1978, kufuatia kifo cha rais wa kwanza, Jomo Kenyatta.

Hadi kifo chake, alikuwa amelazwa katika Nairobi Hospital kwa takriban mwezi mmoja.

Jumanne asubuhi, Rais Uhuru Kenyatta alithibitisha ripoti za kifo cha rais huyo wa zamani na kusema kwamba serikali yake ingetoa taarifa ya kina baadaye.

Baada ya muda mfupi ikulu ya Nairobi ilitoa taarifa rasmi iliyoeleza kwamba kiongozi huyo wa zamani aliaga dunia katika hospitali ya Nairobi akiwa amezungukwa na familia yake.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza alikuwa anaugua nini.

Kupitia kauli ya ikulu, Rais Kenyatta alisema Moi atazikwa kwa heshima zote za kitaifa na akaagiza bendera zote za Kenya zipeperushwe nusu mlingoti hadi siku ya mazishi.

"Marehemu Moi aliongoza Kenya kwa utaratibu hadi ikarejelea mfumo wa vyama vingi vya kisiasa na pia kupitia changamoto nyingi hadi pale alipopokeza mamlaka kwa mrithi wake kwa njia ya amani mnamo mwaka wa 2002," alisema Kenyatta.

Moi, ambaye alizaliwa tarehe 2 mwezi Septemba mwaka wa 1924, alikuwa makamu wa rais kuanzia mwaka wa 1967 hadi mwaka wa 1978 alipochukua hatamu za uongozi.

Rais huyo atakumbukwa kwa juhudi zke za kuimarisha chama kilichotawala wakati huo, Kenya African National Union (KANU), ambacho kwa miaka mingi kilikuwa na umaarufu mkubwa katika pembe nyingi za nchi, hata baada yake kukubali kurejelewa kwa mfumo wa vyama vingi.

Hata hivyo, utawala wake mara kwa mara ulikosolewa vikali na serikali za mataifa ya Magharibi, wapinzani, wanaharakati na watatezi wa haki za binadamu.

Kufuatia kifo chake, Wakenya walikuwa na hisia mseto. Ingawa Rais Kenyatta alimsifu kama"kiongozi mzalendo aliyeitumikia Kenya na bara nzima la Afrika," wengine walikuwa na mtazamo tofauti.

Oduor Ong'wen, alisema kwamba Moi atakumbukwa kama kiongozi aliyeminya uhuru wa wanaharakati wa kutatea haki.

"Mwaka wa 1986 nilikamatwa na kufungwa kwa mika minne. Hivyo ndivyo mimi na wengine tulivyotendewa," alisema Ong'wen kwenye mahojiano na Sauti ya Amerika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Moi pia alishutumiwa kwa uongozi wa kidhalimu na uliogubikwa na ufisadi huku baadhi ya Wakenya wakisema utawala wake ulikuwa wa kidikteta.


Wachambuzi wanasema wakati wa uongozi wa rais huyo wa zamani, uporaji wa mali ya umma ulikithiri na uchumi wa Kenya kudorora kwa kiwango ambacho hakikuwa kimeshuhudiwa hapo awali.

Mnamo mwishoni mwa miaka ya tisini, Marekani na nchi zingine za Magharibi zilimshinikiza Moi kutowania tena urais na baadaye akatangaza kwamba angestaafu kutoka kwa siasa baada ya muhula huo kumalizika.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2002, mgombea urais kwa tikiti ya muungano wa vyama vya upinzani (Narc), Mwai Kibaki, alimshutumu Moi "kwa uwongozi wa mabavu na uliokosa subira na uvumilivu kwa wakosoaji wake."

Lakini sio wote waliomuona Moi kama kiongozi mbaya. Jane Komen aliiambia Sauti ya Amerika kwamba atamkumbuka kama mtu aliyependa watoto.

"Alisaidia kujenga shule nyingi sana," alisema.

XS
SM
MD
LG