Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 10, 2024 Local time: 09:25

Mkutano mkuu wa AU waanza rasmi Addis Ababa


Mousa Faki Mahamat, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 30 wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia. Jumatatu Januari 22, 2018.
Mousa Faki Mahamat, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 30 wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia. Jumatatu Januari 22, 2018.

Mkutano mkuu wa 30 wa Umoja wa Africa (AU) ulifunguliwa rasmi Jumatatu mjini Addis Ababa, Ethiopia, na mwenyekiti wa tume ya umoja huo, Moussa Faki Mahamat.

Mapema Jumatatu, mabalozi wa nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ambao wanawakilisha nchi zao kwenye makao makuu mjini Adis Ababa walihudhuria kikao cha kuratibu masuala muhimu yatakayojadiliwa wakati wa mkutano huo utakaoendelea hadi tarehe 30 mwezi huu.

Baada ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano huo, mabalozi hao waliendelea na kikao chao ambacho kitafuatiwa na kile cha baraza kuu la Umoja huo, kitakachohudhuriwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa AU.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "kupambana na ufisadi." Mahamat alisema kuwa tume ya Umoja wa Afrika inalipa umuhimu mkubwa suala hilo hususan kwa sababu ya hali mbaya inayoendelea kuripotiwa ya kukithiri kwa "janga" hilo katika mataifa mengi ya bara hilo.

"Tume hii itafanya kila itakachoweza kuunga mkono maamuzi yoyote yatakayofikiwa kuhusiana na suala hili muhimu, lakini ni lazima nisisitize kwamba, mwisho wa yote, ni jukumu la mataifa binafsi kukabiliana na ufisadi," aliongeza.

Wanaohudhuria mkutano wa 30 wa Umopja wa Afrika wasimama kwenye ukumbi wa Mandera ili kupigwa picha ya pamoja. Jumatatu, Januari 22, 2018.
Wanaohudhuria mkutano wa 30 wa Umopja wa Afrika wasimama kwenye ukumbi wa Mandera ili kupigwa picha ya pamoja. Jumatatu, Januari 22, 2018.

Wakati wa ufunguzi huo, Mwenyekiti huyo alisema ni wakati muafaka kwa taasisi zote za Umoja wa Afrika kutafakari yale yaliyoweza kutekelezwa na yale ambayo hayajatimizwa na tume hiyo, katika kipindi cha miezi sita tangu mkutano wa mwisho ulipofanyika mwaka jana.

Mahamat alisema moja ya makubaliano muhimu yanayotarajiwa wakati wa kikao cha mwaka huu ni kuhusu azimio la kuwa na hati ya kusafiria kwa raia wa bara la Afrika kutoka nchi moja ya Afrika hadi nyingine bila pingamizi.

"Hii ni hatua ambayo wakati wake umefika. Hatimaye Waafrika wataacha kuwa wageni kwenye bara lao huku wageni kutoka nchi za nje wakitembea bila vizingiti vyovyote," alisema Mahamat.

Alisema kuwa kongamano la mwaka huu pia litashuhudia uzinduzi wa mradi wa usafiri wa anga wa pamoja katika bara la Afrika kufuatia azimio la mwaka 1999 la Yamoussoukro, Ivory Coast.

Tayari nchi 23 zimetia saini makubaliano hayo zikiwemo Kenya na Rwanda katika kanda ya Afrika Mashariki.

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na njia mpya za kuimarisha kilimo barani Afrika, Sayansi na Teknolojia, uongozi bora na kadhalika.

Mkutano huo pia utajadili pendekezo la mwaka wa 2017 kuhusu haja ya kufanya mabadiliko makubwa ya kitaasisi kwa umoja huo.

Mkutano huo unafayika wiki moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuripotiwa kutumia maneno ya matusi yaliyolenga nchi za bara la Afrika na Haiti, na kupelekea Umoja wa Afrika kutuma ujumbe kwa Trump, ukimtaka aombe msamaha.

XS
SM
MD
LG