Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Februari 12, 2025 Local time: 06:49

Mkutano wa Paris: Mataifa tajiri duniani yakamilisha mpango wa kusaidia mataifa yanayo endelea


Mwanaharakati wa mazingira kutoka Uganda Vanessa Nakate akihutubia mkutano wa viongozi wa Paris.
Mwanaharakati wa mazingira kutoka Uganda Vanessa Nakate akihutubia mkutano wa viongozi wa Paris.

Mataifa tajiri duniani yamekamilisha mpango uliokuwa unasubiriwa kwa muda mrefu wa kuyasaidia mataifa yanayoendelea kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akizungumza katika siku ya pili na ya mwisho ya mkutano wa viongozi juu ya mageuzi ya mfumo wa fedha duniani na mabadiliko ya hali ya hewa, Rais wa Ufaransa alisema kwamba wamekamilisha mpango wa kutoa dola bilioni 100 walizoahidi wakati wa mkutano wa Paris mwaka 2015.

Akizungumza katika kikao cha kufunga mkutano huo wa siku mbili uliohudhuriwa na karibu viongozi 40, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kwamba viongozi wamekubaliana kikamilifu juu ya kufanya mageuzi katika mashirika ya kimataifa ya fedha, Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF.

Rais Emannuel Macron
Rais Emannuel Macron

Viongozi wengine pia wamesema wanaunga mkono wazo la kufanya mageuzi katika makubaliano yaliyounda Benki Kuu ya Dunia na IMF yanayofahamika kama taasisi za Bretton Woods zilizoundwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, zinazoongozwa zaidi na mataifa ya Magharibi.

Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen amepongeza ushirikiano uliopatikana wakati wa mkutano kuweza kufikia maridhiano hayo.

Janet Yellen Waziri wa fedha wa Marekani alieleza: "Tumeweza kufikia maridhiano kwenye mkutano huu, tumeweza kuwa na lengo la pamoja la kuhakikisha tuna sayari itakayostawi kwa mafanikio zaidi na kutuwezesha kuishi kwa afya bora. Ni dhahiri pia kuna ari ya kisiasa na dhamira ya dhati kufanya kazi kwa ushirikiano wa kimataifa ili kugeuza ahadi zetu kuwa vitendo."

Mkutano huo wa Paris ulikuwa na lengo pia la kuongeza fedha kwa mataifa yenye kipato ya chini na mipango ya kugharimia athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Licha ya maridhiano hayo mataifa maskini yangali yanasema msaada huo ni mdogo bado kutokana na majanga yanayojitokeza.

Hata hivyo rais wa Ghana Nana Akufo-Addo, hakukubaliana na wazo hilo akisema katika bara la Afrika kuna fedha nyingi lakini zinatumiwa vibaya na kuporwa na kupelekwa nchi za nje.

Rais Nana Akufo Addo
Rais Nana Akufo Addo

Nana Akufo –Addo Rais wa Ghana alisema: Ufadhili kweli ni changamoto kubwa kwa nchi za Kiafrika kuweza kutekeleza mipango ya kukabiliana na mzozo wa hali ya hewa. Lakini tunafedha nyingi sana kwenye bara letu ambazo zinaweza kutumika. Mimi ninazungumzia kiwango kikubwa mno cha fedha ambacho kwa bahati mbaya kinasafirishwa nje ya nchi kwa njia haramu.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwa upande wake amesisitiza juu ya haja ya kuheshimu ahadi zinazotolewa kuhusu msaada wa maendeleo na kugharimia masuala ya hali ya hewa.

Olaf Scholz Kansela wa Ujerumani alisema: Kuna malengo mengi yaliokubaliwa katika mikutano ya miaka ya nyuma kufuatia makubaliano ya Paris. Nadhani kutakuwepo na ahadi zaidi zitakazotolewa katika miaka ijayo. Lakini ni muhimu kwa sisi kufanya kitu cha maana, kinachoweza kufanya kazi. Kwa upande wetu sisi Wajerumani tutaendelea kuwa mstari wa mbele katika kugharimia maendeleo endelevu."

Kwenye mkutano huo Mkurugenzi wa IMF Kristalina Georgieva alitoa habari za kutia moyo aliposema kwamba shirika lake limefikia lengo lake la kuchangisha dola bilioni 100 kusaidia mataifa maskini kukabiliana na mzigo wao wa madeni.

Kristalina Georgieva
Kristalina Georgieva

Benki ya Dunia nayo imesema inafanya kazi kupunguza gharama za kukopesha kwa mataifa yanayokumbwa na majanga asilia.

Wanaharakati kwa upande wao hawakuridhika bado na matokeo wakiyataka mataifa kusitisha matumizi ya mafuta ghafi na wakisema fedha zinazotolewa hazitoshi kusafisha mazingira na kukabiliana na umaskini duniani.

Chanzo cha habari hii ni mashirika ya habari ya AFP na Reuters.

Forum

XS
SM
MD
LG