Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:14

Mara ya ‘mwisho’ kwa Raila, mara ya kwanza kwa Ruto


Watu wamejipanga kupiga kura katika Shule ya Msingi ya Moi avenue Nairobi, Kenya, Tuesday, Aug. 9, 2022.
Watu wamejipanga kupiga kura katika Shule ya Msingi ya Moi avenue Nairobi, Kenya, Tuesday, Aug. 9, 2022.

Uchaguzi mkuu wa Kenya unaofanyika hii leo umetajwa kuwa wenye ushindani mkali sana, kama ilivyokuwa mwaka 2007.

Ukusanyaji maoni na wachambuzi wa siasa wanasema kwamba kinyang’anyiro kikali ni kati ya naibu rais Dr. William Ruto na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Wapiga kura milioni 22 wamejiandikisha kupiga kura hii leo.

Raila Odinga mwenye umri wa miaka 77, anagombea urais kwa mara ya tano. Ameshindwa mara 4. Huenda hii ndio mara yake ya mwisho kugombea nafasi hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Dr. William Ruto mwenye umri wa miaka 55 kugombea urais.

Historia wanayoweka Ruto na Raila katika uchaguzi wa leo

Iwapo Dr. William Ruto anashinda uchaguzi wa leo, ataingia katika historia kama mgombea wa kwanza wa rais kushinda katika jaribio la kwanza nchini Kenya.

Iwapo anashindwa, itakuwa mara ya kwanza kwa Ruto kupoteza uchaguzi tangu mwaka 1997 alipogombea kiti cha ubunge cha Eldoret North na kumshinda mfanyabiashara na mwanasiasa maarufu Reuben Chesire.

Kwa Raila Odinga, iwapo anashinda, atakuwa amevunja laana ya kushindwa katika uchaguzi wa urais ambapo aliwania mwaka 1997, 2007, 2013 na 2017.

Njia gani kwa Raila akishindwa, Ruto akishinda?

Endapo Ruto anamshinda Raila hii leo, itabidi Raila asubiri hadi miaka 5 ijayo, atakapokuwa na umri wa miaka 82 ndipo agombea kwa mara nyingine. Hii ndio nafasi pekee aliyo nayo. Wachambuzi wa siasa wamesema kwamba akishindwa hii leo, huenda basi kiu yake ya kutawala Kenya itakuwa imemponyoka milele.

Ruto akishinda, wachambauzi wamesema kwamba kuna uwezekano akatawala Kenya mihula miwili, jumla ya miaka 10. Wakati anamaliza mihula miwili, Raila atakuwa na umri wa miaka 87.

Kampeni ya Raila, Ruto

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, 2013 na 2017, kampeni ya Raila ilizingatia sana namna ya kuwasaidia watu maskini na kuhakikisha kwamba raslimali za kitaifa zinagawanywa kwa usawa. Raila alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na ahadi hizo kwa mamilioni ya wakenya ambao kwa miaka mingi wanahisi kwamba pengo kati ya matajiri na maskini linaendelea kuongezeka.

Katika uchaguzi huu, Raila ameonekana kutokuwa na ahadi maalum na badala yake, Ruto ametumia mfano wa ahadi alizokuwa akitumia Raila katika miaka iliyopita, na amewaahidi wakenya kwamba atainua uchumi wa Kenya kwa kuzingatia watu wa kipato cha chini. Mfumo wake Ruto umefahamika sana Kenya kama ‘bottom up’.

Raila, kwa kushirikiana na rais Uhuru Kenyatta, amehusishwa zaidi na watu tajiri ‘wasiojali maslahi ya maskini’ nchini Kenya.

Marafiki na tena maadui kisiasa

Raila Odinga na William Ruto walikuwa katika chama kimoja cha Orange Democratic Party wakati wa uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali wa mwaka 2007.

Uhasama wao kisiasa ulianza baada ya Raila kumfuta kazi Ruto kama waziri wa kilimo, wakati huo akiwa waziri mkuu katika serikali ya muungano na aliyekuwa hayati rais Mwai Kibaki.

Ruto aliunda chama chake cha URP huku Odinga akibaki ODM.

Baadaye Ruto aliungana na Uhuru Kenyatta na kuunda chama cha Jubilee na kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, 2017 huku Odinga akishindwa.

Wengine waliokuwa pamoja na Odinga na ambao sasa wanashirikiana na Ruto ni pamoja na Moses Wetangula na Musalia Mudavadi.

Nani atakuwa rais nan ani atakuwa kiongozi wa upinzani?

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ina muda wa siku 7 kuatangaza mshindi wa urais. Hii ina maana kwamba IEBC ina muda hadi tarehe Agosti 16 2022 kutangaza mshindi wa urais ambaye ni lazima apate asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa, na kura moja ya ziada. Ni lazima pia mshindi apate asilimia 25 ya kura katika kaunti 24 kati ya kaunti zote 47.

Mtu yeyote anaweza kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani na uchaguzi kurudiwa iwapo mahakama itapokea ushahidi wa kutosha kupelekea uchaguzi kufutiliwa mbali.

Odinga amekuwa mahakamani mara kadhaa kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu. Alipinga ushindi wa rais Uhuru Kenyatta mwaka 2013 na 2017.

XS
SM
MD
LG