Badala yake, mahakama hiyo imeiamuru tume ya uchaguzi IEBC kutumia tu daftari la karatasi iwapo mfumo wa digital utakosa kufanya kazi, na hivyo uchaguzi huo ufanyike kwa njia ya digitali.
Majaji Fred Ochieng, Luka Kimaru na Paul Gachoka, wamesema kwamba chama cha United Democratic Alliance UDA, cha naibu rais William Ruto, kimetoa ushahidi wa kuridhisha kwamba uamuzi wa mahakama ya chini wa kutaka daftari la karatasi litumike, ulikuwa ni makosa.
Wakili wa chama UDA Elias Mutuma amesema kwamba kuna uwezekano wa kutokea hali ya kuchangangikiwa kuhusu namna ya kutambua wapiga kura wakati wa zoezi hilo.
Chama cha UDA kimesema kwamba kuna “uwezekano mkubwa wa daftari la karatasi kutumika visivyo kwa vile halina ulinzi wa aina yoyote ikilinganishwa na daftari la digitali.”
Muungano wa Azimio, wa waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga, pamoja na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali, walikuwa wameungwa na mahakama ya chini kwamba daftari la karatasi la kuwatambua wapiga kura litumike kwa wakati mmoja na mfumo wa digitali.
Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki aliiambia mahakama kwamba ni vyema daftari la karatasi liwepo kama mfumo wa pili iwapo mfumo wa digitali utakosa kufanya kazi.
Lakini chama cha William Ruto kimeiambia mahakama kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa wasimamizi wa uchaguzi kupigia kura watu ambao hawajafika kwenye kituo kupiga kura na hakutakuwa na uwezo wowote kujua idadi ya wapiga kura waliojitokeza.