Kwenye fukwe za ziwa Malawi umaskini na uhaba wa chakula ni matatizo sugu, kutokana na kushuka kwa samaki wanaopatikana katika ziwa hilo.
Wanawake wanakabiliwa na njaa, au wanajaribu kuwapatia chakula familia zao, mara nyingine wanageukia wanaume wavuvi ili kupata samaki ili wawe na walau chakula na matokeo yake ni kulazimika kufanya ngono.
Wanawake wanabeba ndoo kila asubuhi kwenda kununua samaki kwenye ziwa Malawi na hiyo ndiyo kawaida katika eneo la Makawa.
Jambo ambalo kidogo si la kufurahisha ni kwamba wanawake wengi wanajikuta wakilipia samaki hao kwa kutoa ngono.
Cecilia Iman ni katibu katika kamati ya eneo la Village Beach, anayehusika katika huduma za rasilimali za ziwa katika eneo hilo.
Anaeleza : "Jambo hili linatokea hapa. Wavuvi wengi wanafika ziwani wakiwa na lengo kuwa watapa wanawake hapa. Lakini uhusiano wao haudumu, wanachofanya ni kuwaletea matatizo wanawake wa kijijini."
Pia anasema kuwa wanawake wanarubuniwa kujiingiza katika biashara ya ngono kwa vile hawana fedha za kununua samaki, au wanapokubali makubaliano yanayotolewa na wavuvi wanasema maafisa.
Iman anasema kwa mfano, mtu anaweza kuwa na kwacha za Malawi 2,000 lakini anataka baadhi ya fedha hizo anunulie samaki, akifika huko muuza samani anampa samaki bure. Ukichanganya kuwa hajakula jana usiku yeye pamoja na mtoto wake, ataishia kukubali wazo la mvuvi ambalo matokeo yake inakuwa ni kufanya kitendo ambacho hakutarajia.
Utaratibu huu umewasababisha madhila wanawake wengi
"Kama maambukizi ya HIV yanaongekeza katika eneo letu, kwa kiasi kikubwa kwasababu ya wavuvi wetu. Wanawake wana shida sana ya samaki. Na pia wavuvi wengi wanawatia mimba wanawake halafu wanakimbia, na kuwaacha wakihangaika na kuwahudumia watoto," anasema Iman.
Ingawaje malipo ya ngono kati ya wanawake na wavuvi katika ziwa Malawi yamekithiri, unyanyapaa na ubaguzi unafanya iwe vigumu kuwatambua wale waliohusika.
Mwana kijiji mmoja, Laika Atibu, ameiambia VOA hawezi kuwaruhusu wavuvi wamrubuni kwa samaki.
"Sitaruhusu hilo. Najaribu kufanya kila niwezalo kwa kufanya kazi ili niweze kupata hela za kununulia samaki. Kwasababu nakhofia , kama nikifanya hivi, naweza kupata maambukizi ya HIV, nani atawalisha wanangu, kwasababu mimi ndiyo mzazi pekee ambaye ninawahudumia," anaeleza Atibu.
Wavuvi wanajiweka kando na suala hili
Yalid Nkhoma anasema kutumia samaki kama chombo cha kurubuni ni sawa na kuwanyanyasa wanawake.
Nkhoma: "Hatufanyi hivyo. Kama mwanamke hana hela za kutosha kununua samaki, hatuwaambii kwamba wafanye chochote na sisi.
Tafiti tofauti zinaonyesha kwamba ngono kwa samaki nchini Malawi ni jambo la kawaida kati ya miezi ya Disemba na Machi kwa sababu ni kipindi ambacho nchi imepigwa vibaya na uhaba mkubwa wa chakula.
Kuzuia tatizo hili, viongozi wa jamii wameanzisha uwezeshaji wakiuchumi kwa wanawake, ikiwemo mpango wa mikopo, kuhakikisha kuwa wana vyanzo vyao vya mapato na wasitegemee wavuvi kuepukana na njaa.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Khadija Riyami, Washington, DC