Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 12:32

Mahakama yatupilia mbali rufaa ya DPP dhidi ya Mbowe, Matiko


Mbowe na Matiku wa Chadema wakiwa mahakamani.
Mbowe na Matiku wa Chadema wakiwa mahakamani.

Mahakama ya Rufaa imeagiza Ijumaa jalada la kesi lirejeshwe Mahakama Kuu nchini Tanzania, kwa ajili ya kuendelea kusikiliza maombi ya washtakiwa ya kutenguliwa kwa dhamana yao.

Mahakama hiyo imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini iliyokuwa inapinga Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko kupatiwa dhamana.

Jopo la majaji limesema rufaa ya DPP haina nguvu ya hoja na kwamba Jaji Sam Rumanyika alikuwa sahihi kukubali kusikiliza rufani ya kupinga kutenguliwa dhamana ya washtakiwa hao.

Akisoma hukumu hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Sylvester Kainda alisema kuwa rufaa ya DPP haikidhi matakwa ya Mahakama ya Rufaa kwa sababu haikuwa sahihi kuweka pingamizi huku ikijua Mahakama Kuu tayari ilikuwa imepewa mamlaka.

''Haikuwa sahihi kwa DPP kuleta pingamizi wakati wanajua mamlaka ambayo Mahakama Kuu imepewa na hiki sio kitendo kizuri hivyo, rufaa hii haina msingi na jalada liendelee na usikilizwaji wake Mahakama Kuu,'' alieleza Kainda.

Alisema ni kweli rufaa iliyokatwa na Mbowe na Matiko, ilikuwa chini ya hati ya dharura na kwamba kumbukumbu za mwenendo wa shauri hilo kutoka mahakama ya chini (Kisutu) hazikuwa zimeambatanishwa.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, mwaka 2018 baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo pamoja na viongozi wengine saba wa chama hicho.

Uamuzi huo ulitolewa na jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Stella Mgasha, Mwanaisha Kwariko na Gerald Ndika baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili zilizofikishwa Februari 18, 2018.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Paul Kadushi na Mawakili wa Serikali, Samon, Salum Msemo walipinga rufaa hiyo ikiwemo Jaji kukosea kupanga kusikilizwa kwa rufaa kinyume na kifungu cha 362 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG