Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 20, 2024 Local time: 12:17

Magufuli asema Tanzania imepunguza wagonjwa wa Covid-19


Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

Rais wa Tanzania John Magufuli anasema wagonjwa wa corona wamepungua nchini humo na anafikiria kufungua shughuli za masomo ya vyuo vikuu na michezo katika siku chache zijazo.

Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la kilutheri mkoani Geita, magharibi mwa Tanzania, Rais Magufuli alitoa idadi za wagonjwa wachache wa Covid-19 waliobaki katika hospitali mbali mbali nchini humo na kusema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na sala na maombi kwa Mwenyezi Mungu.

Siku moja baada ya Kenya kufunga mpaka wake na Tanzania kwa siku 30 kuzuia ueneaji wa maambuziki ya Covid-19, Rais Magufuli amesema Tanzania haitafunga mipaka yake kwa sababu kwa kufanya hivyo itaathiri nchi jirani na biashara za Tanzania.

“Ndio maana ndugu zangu sikufunga mipaka niliheshimu majirani zangu, tumezungukwa na karibu nchi nane, ukizifungia maana yake umezinyima uchumi wao kuna baadhi ya nchi wanategemea vyakula vya Tanzania''.

Bila kuitaja Kenya hotuba ya Rais Magufuli ilielekea kujibu hatua ya Kenya kufunga mpaka na kujibu malalamiko yanayoelezwa kutokea katika mipaka ya Tanzania na jirani zake kwa waendesha magari ya mizigo.

Magufuli alisisitiza kuwa Tanzania itafanya inachojua na haitashurutishwa na watu wa nje kuchukua hatua zaidi ya ilivyofanya tangu mgonjwa wa kwanza wa Covid-19 kupatikana nchini humo mwezi March.

Rais Magufuli amekuwa akisisitiza maombi katika kupambana na Covid-19 na aliwashukuru viongozi wa kidini nchini humo kwa kuwacha nyumba za ibada wazi ili watu waendelee kuomba kwa Mungu kuondokewa na janga na corona.

Katika hotuba ya Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Afya Tanzania na madaktari kuwa hata watu watakaofariki kwa ugonjwa wa Covid-19 watolewe kwa ndugu zao ili wapewe heshima ya maziko ya kawaida kwa binadamu.

Tanzania imekuwa ikilaumiwa kimataifa kwa kutochukua hatua kali za masharti ya kupambana na virusi vya corona kama inavyofanyika katika nchi za jirani na nyinginezo duniani.

Mara ya mwisho Tanzania kutoa takwimu za Covid-19 ilikuwa Aprili 29 na idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo hadi sasa imesimama kwenye 509.

Upinzani Wajibu

Katika hotuba iliyopangwa tangu awali Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CHADEMA Freeman Mbowe alijibu baadhi ya hoja za Rais Magufuli na kusema njia inayotumiwa na Tanzania katika kupambana na Covid-19 inaiweka nchi hiyo katika hatari.

Freeman Mbowe
Freeman Mbowe

Bila kutoa takwimu Mbowe alisema Tanzania bado inakabiliwa vikali na ugonjwa Covid-19. Aliongeza kuwa serikali ya Tanzania ingali na nafasi ya kuchukua baadhi ya hatua zaidi hata kwa kiwango kidogo ili kukabiliana na janga hilo badala ya kuficha ukweli.

Mbowe alitoa rai rasmi kwa Rais Magufuli akimsihi kwamba washauri wake wanamwogopa na hawamuelezi hali halisi ya ugonjwa huo nchini Tanzania.

Kiongozi huyu amesema kuweko kwa taarifa za nchi jirani kufunga mipaka na hata kuzuia Watanzania kuingia katika nchi hizo au kuwekewa utaratibu mpya wa masharti inatokana na kukataa ushauri wa kisayansi.

Siku nyingi huko nyuma niliwahi kutoa tahadhari tusipokubali kufanya 'Lockdown' (amri ya kutotoka nje) hata Partial lockdown (hata ikiwa ni sehemu tu ya amri hiyo) tutakuwa Lockedout (tutatengwa).

Amesema "mwanzoni tulizungumza kujifunza kutoka uzoefu wa nchi nyingine katika kupambana na janga la corona, sasa tunazungumzwa na nchi nyingine kama kielelezo hasi cha vita dhidi ya janga la corona Afrika na duniani.

"Mikutano ya jumuiya ya Afrika Mashariki ya viongozi wa nchi hizo wakati sisi tukiwa hatuna wawakilishi ndio mwanzo wa 'Lockout' (kutengwa)," ameeleza Mbowe.

Ameongeza kuwa "Lakini inawezekana kati yetu kukawa na wale wako katika 'state of denial' hali ya kukanusha hawataki kukubali..." tukaruhusu ugonjwa kuenea mno na kuuwa wapendwa wetu.Tulidhani tunalinda uchumi wetu, tulisahau kulinda uhai wa watu wetu."

"Sasa corona inaendelea kutula sote. Inakula uchumi wetu tupende tusipende na inatafuna uhai wetu. Hiyo ndio hali halisi mwenye macho haambiwi ona," alisisitiza.

XS
SM
MD
LG