Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 23, 2023 Local time: 01:06

Kimbunga Freddy: Watu zaidi ya 200 wapoteza maisha


Mwanamume aliyejeruhiwa akisaidiwa huko Blantyre Malawi, Machi 13, 2023. Picha na shirika la habari la AP/Thoko Chikondi.

Idadi ya vifo vilivyo kutokana na Kimbunga Freddy nchini Malawi na Msumbiji imeongezeka na kuvuka watu 200 Jumanne, baada ya dhoruba hiyo iliyovunja rekodi na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi wakati kilipopiga kwa mara ya pili huko Afrika katika kipindi cha chini ya wiki tatu.

Wafanyakazi wa uokoaji walionya kwamba huenda wakawepo waathirika zaidi wakati wakiendelea na msako katika vitongoji vilivyoharibiwa, kuwatafuta manusura hata pale matumanini yalipopungua.

Dhoruba kali imelikumba tena eneo hilo la kusini mashariki mwa Afrika mwishoni mwa wiki, Ikiwa ni mara yake ya pili kupiga tangu mwishoni mwa mwezi Februari baada ya kutokea Australia na kuvuka Bahari ya Hindi.

Serikali ya Malawi ilisema takriban watu 190 wamefariki na wengine 584 kujeruhiwa wakati watu 37 hawajulikani walipo. Wakati huo huo mamlaka ya nchi jirani ya Msumbiji iliripoti vifo vya watu 20 na majeruhi 24.

"Hali ni mbaya sana," alisema Guilherme Botelho ambaye ni mratibu wa mradi wa dharura wa shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) nchini Malawi.

"Kuna majeruhi wengi, waliojeruhiwa, waliopotea au kufariki, na idadi hii inatarajiwa kuongezeka katika siku zijazo." alisema.

Watu wengi wameangamia katika maporomoko ya matope yaliyosomba nyumba mjini Blantyre, mji mkuu wa kibiashara nchini Malawi.

Kote nchini humo takriban watu 59,000 wameathiriwa, na zaidi ya 19,000 wamekoseshwa makazi, huku wengi wao kwa sasa wanajihifadhi kwenye shule na makanisa.

Freddy bado inasababisha mvua na upepo katika maeneo hayo ya kusini mwa Malawi siku ya Jumanne, lakini hali inatarajiwa kuwa shwari kuanzia Jumatano jioni, kulingana na kitengo cha huduma za hali ya hewa nchini humo.

Huko Chilobwe, kitongoji kidogo nje ya Blantyre, waathirika walipigwa na butwaa wakiangalia nyumba na majengo mengine yaliyo yaliobomolewa na kuwa tambarare wakati huku mvua ikiendelea kunyesha.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG