Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 22, 2024 Local time: 10:44

Kimbunga Freddy kutua Msumbiji, watu wachukua tahadhari


Wanaume wakitembea kwenye barabara iliyofurika katika ufukwe wa Kisiwa cha Mauritius kilichopo katika bahari ya Hindi Februari 20, 2023. Picha na AP Photo/L'express Maurice.
Wanaume wakitembea kwenye barabara iliyofurika katika ufukwe wa Kisiwa cha Mauritius kilichopo katika bahari ya Hindi Februari 20, 2023. Picha na AP Photo/L'express Maurice.

Mamlaka nchini Msumbiji iliwataka watu kutafuta makazi na bandari kuu ya Beira imefungwa siku ya Ijumaa, wakati dhoruba ya kitropiki Freddy ikitarajiwa kutua katika eneo hilo hivi karibuni

Shirika la utabiri wa hali ya hewa la Ufaransa ambalo lina kituo cha kufuatilia vimbunga katika kisiwa cha La Reunion kilichopo katika bahari ya Hindi, kimesema kimbunga Feddy kinatarajiwa kutua karibu na mji wa kitalii wa Vilankulo ulioko kusini mwa jimbo la Inhambane nchini Msumbiji nyakati za mchana.

Katika picha iliyochapishwa na afisa wa eneo la Vilankulo, Edmundo Galiza Matos Junior katika mtandao wa Facebook inaonyesha watu wakichukua hifadhi kwenye shule na picha za video zikionyesha upepo mkali ukipiga eneo la pwani.

Taarifa ya kampuni ya Cornelder de Moçambique, inayofanya kazi ya kushughulikia mizigo katika vituo vya bandari ya Beira, imesema kuwa bandari itafungwa siku ya Ijumaa mpaka jioni kutegemea na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwenye tovuti Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema mpaka watu millioni 1.75 wanaweza kuathiriwa na dhoruba na mafuriko makubwa.

“Katika siku zijazo mvua kubwa inatarajiwa kunyesha katika majimbo ya Gaza, Manica, Maputo, Inhambane na Sofala. Umoja wa Mataifa na washirika wetu wanasaidia juhudi zinazoongozwa na serikali za kukabiliana na dhoruba. Tumepeleka wafanyakazi katika majimbo ya Inhambane na Gaza na timu zetu zimejiandaa kufanya tathmini ya mahitaji," ilisema OCHA.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.

XS
SM
MD
LG