Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 23, 2024 Local time: 16:05

Kenyatta azitaka serikali za kaunti kupanda miti na kulinda mazingira


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika ufunguzi wa kongamano la saba la kila mwaka la Ugatuzi nchini humo linaloendelea katika kaunti ya Makueni mashariki mwa nchi hiyo, ameeleza kuwa serikali yake imepiga hatua muhimu na thabiti kukabili athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkutano huo unaojumuisha kaunti 47 kwenye jukwaa moja unaangazia athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini Kenya na jinsi serikali hizo na mashirika binafsi yanavyoweza kushirikiana katika ubia kukabili athari zake kwa maisha ya raia, mazingira na mifugo.

Zaidi ya wajumbe 3,000 miongoni mwao wakiwa ni wakuu wa serikali, wataalamu, wafanyabiashara, wanaharakati, wafadhili na wakuu wa mashirika mbalimbali ya kimataifa, wiki hii wapo kwenye jukwaa linaloangazia mafanikio ya ugatuzi nchini Kenya, kufanikisha mkakati wa ugavi sawa wa raslimali za kitaifa na mafanikio yaliyofikiwa kupitia mfumo huo wa kufikisha rasilimali mashinani.

Mkutano huu umejengeka kwenye maudhui ya mabadiliko ya hali ya hewa, kuzingatia utawala wa mawanda mbalimbali na ngazi za serikali kuchukua hatua za kukabili athari ya mabadiliko hayo kupitia ufikiaji wa mkakati thabiti zaidi wenye vitendo.

Rais Kenyatta ameeleza kuwa serikali yake imejiunga na jukwaa la kimataifa hasa kupitia maafikiano ya ahadi zilizotolewa na viongozi kwenye mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa COP26 huko Glasgow, Scotland na hatua kamilifu za kupunguza kuongezeka kwa joto hadi chini ya nyuzi joto mbili kiwango kilichowekwa kwenye mkataba wa Paris wa 2015.

Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa COP26 wa UN, Glasgow, Scotland, Nov. 13, 2021.
Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa COP26 wa UN, Glasgow, Scotland, Nov. 13, 2021.

Rais Kenyatta aliongeza : “Mabadiliko ya hali ya hewa si tatizo la siku zijazo bali ni tishio la sasa na kubwa kwa nchi zote duniani. Mabadiliko ya hali ya hewa yanaleta tishio kwa Kenya ingawa jukumu letu katika kuendeleza tatizo ni kidogo - tunachangia chini ya 1% ya uzalishaji wa sasa wa gesi chafu duniani, lakini sisi ndio tunaoathirika zaidi na tatizo hili.”

Kwa miaka miwili iliyopita, Kenya imeshuhudia hali mbaya ya kuzuka kwa nzige kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka ishirini na tano, iliyosababisha uhaba wa chakula kwa raia wengi.

Aidha, Kenya pia imeshuhudia kuongezeka kwa viwango vya maji kwenye Ziwa Victoria na maziwa yaliopo kwenye eneo la Rift Valley pamoja na bwala la Turkwel na kusababisha mafuriko na kuwaathiri karibu watu laki nne kwenye kaunti kumi na tatu.

Kwa sasa watu milioni 2.5 nchini Kenya katika kaunti 23 wanakabiliwa na baa la njaa kwa sababu ya ukame.

Kenyatta ameeleza kuwa ni lazima pawepo na jitihada za pamoja kuongeza kiwango cha misitu kwenye ardhi ya Kenya kutoka asilimia 6.9% hadi asilimia 10% ifikapo mwaka 2022.

Aidha, Kenyatta amesisitiza kuwa serikali kupitia wizara ya mazingira inalenga kusambaza angalau miche milioni 42.5 katika kila kaunti, kutimiza lengo lake la kufikisha jumla ya miche bilioni mbili inayohitajika ili Kenya kufikia asilimia 10 ya misitu.

Rais alisema : “Ni muhimu kwamba ngazi mbili za serikali zifanye kazi kwa karibu ikiwa tunataka kutekeleza malengo yetu kwa ufanisi.”

James Koinare, mtaalam wa masuala yanayofungamana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini Kenya anaeleza kuwa ngazi hizi mbili za serikali zinastahili kuonyesha vitendo wala si majukwaa ya kuzungumza tu.

Ulimwenguni, Kenya imeorodheshwa kuwa nchi ya 31 iliyo hatarini zaidi kwa mabadiliko ya hali ya hewa, ameeleza Koinare.

Athari za mabadiliko ya hali ya hewa husababisha hasara ya takribani 3% ya Pato la Taifa kila mwaka.

Kenya inaeleza kuwa imejitolea kupunguza utoaji wake wa gesi chafu kwa asilimia 32 kufikia 2030. Hii itagharimu shilingi bilioni 6,874.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi.

XS
SM
MD
LG