Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 13:24

Kenyatta abuni nafasi mpya katika wizara zote serikalini


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. Aliteua baraza la mawaziri 22 tarehe 26 Januari, 2018.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. Aliteua baraza la mawaziri 22 tarehe 26 Januari, 2018.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Ijumaa alitangaza kwamba ameunda nafasi mpya ya usimamizi kwenye wizara zote na kuteua baadhi ya watu ambao hawakufaulu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana kuchua nyadhifa mbalimbali.

Kenyatta aliunda nafasi ya katibu mkuu wa utawala (Chief Administrative Secretary) kwenye wizara zote 22.

Wakati wa muhula wake wa kwanza, rais huyo alikuwa na mawaziri 18 kwenya baraza lake.

Hata hivyo, kufuatia uchaguzi wa mwaka jana, kumekuwa na shinikizo kumtaka aongeze idadi ya mawaziri, huku baadhi ya wakenya wakisema ni muhimu mno kwake "kutoa nafasi kwa jamii zote za Kenya ili kushiriki serikalini."

Kenyatta aliteua baraza lote la mawaziri takriban mwezi mmoja na nusu tangu kutangazwa mshindi wa urais na mahakama ya juu ya nchi hiyo.

Mapema mwezi huu, alitangaza mawaziri tisa, hatua ambayo ilikosolewa na baadhi ya Wakenya hususan kwa sababu hakutaja hata jina moja la mwanamke kwenye uteuzi huo.

Hata hivyo, orodha iliyotolewa Ijumaa ilikuwa na wanawake sita. Baadhi ya watu waliopoteza nafasi zao kwenye uchaguzi wa Agosti 8, 2017, waliteuliwa aidha kama mawaziri, makatibu wa wizara au mabalozi.

"Baada ya kushauriana na wadaiu mbalimbali, nimeamua kuwateua watu wafuatao kusaidia katika utekelezaji wa kazi za serikali," alisema Kenyatta katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja na vyombo ya habari nchini Kenya.

Mawaziri sita ambao walikuwa wanahudumu katika serikali yake muhula uliopita waliachishwa kazi hiyo na kuteuliwa kuwa mabalozi.

Baada ya Tanzania kukaa kwa muda mrefu bila mwanadiplomasia wa kiwango cha balozi wa Kenya kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa balozi wa Kenya nchini humo Chirau Ali Mwakwere hapo mwaka jana ili kuwania kiti cha ugavana katika uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, sasa Kenyatta amemteua Dan Kazungu, ambaye amekuwa waziri wa madini, kuchukua nafasi hiyo.

Amina Mohamed, ambaye alihudumu kama waziri wa mambo ya nje, amehamishiwa kwenye wizara ya elimu. Wizara ya mambo ya nje sasa imepewa aliyekuwa katibu wa wizara hiyo hiyo, Monica Juma.

Mbunge wa zamani Ababu Namwamba atakuwa baadhi ya watu wa kwanza kuchukua wadhifa mpya kabisa wa katibu mkuu wa utawala.

Haya yanajiri wakati muungano wa upinzani nchini humo (NASA), unashikilia kwamba rais Kenyatta hakuchaguliwa kihalali na kwamba wanachama wake hawamtambui kama rais.

Kiongozi wa muungano huo ameelezea nia yake ya kutaka kuapishwa kama "rais wa wananchi" tarehe 30 mwezi huu.

Balozi wa Kenya katika umoja wa mataifa, Macharia Kamau, ameteuliwa kama katibu wa kudumu katika wizara ya Afya, huku balozi wa Kenya nchini Uingereza Lazarus Amayo akiteuliwa kuchukua nafasi ya Kamau mjini New York.

Walioteuliwa watafika mbele ya kamati ya bunge ili kuidhinishwa au kukataliwa.

Hii ndiyo orodha kamili ya walioteuliwa:

  1. Waziri wa Fedha - Henry Rotich
  2. Waziri wa Afya - Sicily Kariuki
  3. Waziri wa Kawi - Charles Keter
  4. Waziri wa Utalii - Najib Balala
  5. Waziri wa Mambo ya Kigeni - Monica Juma
  6. Waziri wa Elimu - Amina Mohamed
  7. Waziri wa Kilimo - Mwangi Kiunjuri
  8. Waziri wa Viwanda - Aden Mohamed
  9. Waziri wa Ulinzi - Raychelle Omamo
  10. Waziri wa Usalama wa Ndani - Fred Matiang’i
  11. Waziri wa Michezo na Turathi - Rashid Mohamed
  12. Waziri wa Ugatuzi - Eugene Wamalwa
  13. Waziri wa Uchukuzi - James Macharia
  14. Waziri wa Teknolojia - Joe Mucheru
  15. Waziri wa Mazingira na Misitu - Keriako Tobiko
  16. Waziri wa Maji - Simon Chelugui
  17. Waziri wa Ardhi - Farida Karoney
  18. Waziri wa Mafuta na Madini - John Munyes
  19. Waziri wa E.A.C - Peter Munya.
  20. Waziri wa Utumishi kwa Umma,Vijana na Jinsia - Margaret Kobia
  21. Waziri bila kazi mahsusi - Raphael Tuju
  22. Waziri wa Leba - Ukur Yattani

MABALOZI:

Balozi wa Kenya nchini Ufaransa - Judy Wakhungu

Balozi wa Kenya Umoja wa Mataifa(Geneva) - Cleopas Mailu

Balozi wa Kenya nchini Tanzania - Dan Kazungu

Balozi wa Kenya, UNESCO (Paris) - Jacob Kaimenyi

Balozi wa Kenya, UN, New York - Lazarus Amayo

Balozi wa Kenya,Ubelgiji - Phylis Kandie

Balozi wa Kenya,India - Willy Bett

Balozi wa Kenya, Austria - Hassan Wario

Balozi wa Kenya, Uganda - Kiema Kilonzo

-Mwandishi wa Sauti ya Amerika, Kennedy Wandera amechangia ripoti hii.

XS
SM
MD
LG