Upatikanaji viungo

Breaking News

Jumuiya ya kimataifa yatoa wito wa kusitishwa mapigano Libya


Wanajeshi watiifu wa kamanda Khalifa Haftar, wakitoka nje ya mji wa Benghazi kuongeza nguvu ya vikosi vinavyofanya mashambulizi kuingia Tripoli, Libya, Apr. 7, 2019.

Wananchi wa Libya katika mji mkuu wa Tripoli wameandamana Jumatatu ili kupinga mashambulizi yanayofanywa na wanajeshi watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar, kamanda wa jeshi linalodhibiti maeneo ya mashariki ya Libya, LNA.

Kamanda huyo alianzisha mashambulizi mwishoni mwa wiki kwa lengo la kuiondoa serikali ya umoja wa kitaifa (GNA) inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Serikali ya GNA imetangaza hii leo kwamba watu 21 wameuawa katika mapigano Jumapili, huku UN ikieleza kwamba hakuna makubaliano ya kusitisha mapigano hayo yaliyofikiwa.

UN ilitoa wito wa kusitisha mapigano kwa saa mbili Jumapili ili kuruhusu raia na waliojeruhiwa kuondoka.

Marekani nayo imetoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano hayo yanayoendelea nje ya mji wa Tripoli.

Wachambuzi wa masuala ya Libya wanasema wasiwasi wa kuzuka upya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya umeongezeka mishoni mwa wiki.

Hii ni baada ya wanajeshi watiifu kwa kamanda Khalifa Haftar kuvamia kwenye vitongoji vya Tripoli na serikali ya umoja wa kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa kuanzisha mapambano dhidi ya wanajeshi hao wanaosonga mbele.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG