Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Oktoba 05, 2024 Local time: 15:32

Wahamiaji 90 wafa maji Libya


Waokoaji wakiiopoa miili ya wahamiaji waliokufa maji Libya
Waokoaji wakiiopoa miili ya wahamiaji waliokufa maji Libya

Shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM) linasema kiasi cha wahamiaji 90 wamekufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kwenye pwani ya Libya kuzama mapema Ijumaa alfajiri. Wahamiaji wengi wanaaminika kuwa ni raia wa Pakistan.

Idara ya Umoja wa Mataifa ya uhamiaji imesema miili 10 imeripotiwa kuoshwa kwenye fukwe za Libya, ilikuwa ya raia wawili wa Libya na wanane wa Pakistan. Idara hiyo inasema habari kuhusu janga hilo la karibuni bado haieleweki na uchunguzi unaendelea.

Msemaji wa IOM, Olivia Headon yuko nchini Tunisia kufuatilia mkasa huo. Akiongea kwa njia ya simu kutoka mji mkuu, Tunis, ameiambia VOA kuwa wahamiaji inaonekana walikuwa wakifanya safari hatari katika boti ya magendo iliyokuwa na msongamano mkubwa wa watu.

“Hadi hivi sasa, hakujakuwepo na uokozi wowote isipokuwa mtu mmoja ambaye aliokolewa na boti ya uvuvi. Imetokea kwa mvuvi wa Libya na watu wengine wawili walionusurika kuogelea hadi ufukweni. Naamini kwamba walinzi wa pwani wa Libya wanatafuta wengine walionusurika kwa wakati huu,” amesema msemaji Headon.

Libya ni njia kuu kwa wahamiaji ambao wanajaribu kufika nchini Italy. Mwaka jana, Umoja wa Ulaya (EU) kwa kiasi kikubwa ulikosolewa kwa kufanya makubaliano na walinzi wa pwani wa Libya kujaribu kuzuia usafiri katika njia hiyo.

Wahamiaji wengi na wakimbizi hufanya safari hatari kuvuka bahari ya Mediterranean kwenda Italy wakitoka barani Afrika chini ya jangwa la Sahara. Si kawaida kuwa na raia wengi wa Pakistan ambao hutumia njia hiyo na takwimu za IOM zinaonyesha kuwa idadi yao inaongezeka.

Mwaka jana, IOM inasema wahamiaji 3,138 wa Pakistan waliwasili nchini Italy kwa njia ya bahari kutokea Libya. Hii ilikuwani orodha ya 13 ya idadi ya wahamiaji waliowasili mwaka 2017. Mwaka huu, idara hiyo inakadiria kwamba raia 240 wa Pakistan walifika Italy mwezi Januari, na kuwafanya ni idadi kubwa ya raia hao hadi hivi sasa. Ukilinganisha, IOM inaelezea ni raia tisa tu wa Pakistan waliwasili nchini Italy kwa njia bahari mwezi Januari mwaka jana.

Idara hiyo inasema bado haiko bayana nini hasa kinachangia kuhusu ongezeko la wahamiaji kutoka Pakistan.

XS
SM
MD
LG