Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) limebadili makadirio yake kwa kupunguza kiwango cha ukuaji wa uchumi kote duniani kwa 3.6% kwa mwaka 2022, likisema kwamba uvamizi wa Russia nchini Ukraine unatishia ukuaji dhaifu wa uchumi baada ya kutoka kwenye janga la virusi vya Corona.
Mawaziri wa Fedha na maafisa wa uchumi na fedha duniani wanakutana mjini Washington wiki hii kwa mkutano wa kila mwaka wa majira ya machipuko.
Uvamizi wa Russia nchini Ukraine na vikwazo vya nchi za magharibi dhidi ya Moscow, vimeathiri ukuaji wa uchumi na kuharibu biashara kote duniani, na hivyo kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta na kutishia kutokea ukosefu wa chakula, wakati ulimwengu unapitia hali ngumu kujikomoba kutokana na janga la virusi vya Corona.
Pierre Olivier Gourinchas ni Mchumi Mkuu wa IMF anasema hali hii imepelekea Shirika la Fedha la Kimataifa, kubadili makadirio yake ya ukuaji wa uchumi.
Hata kabla ya vita, mfumuko wa bei katika nchi nyingi ulikuwa unaongezeka kutokana na kutokuwepo na uwiano kati ya mahitaji ya bidhaa muhimu na sera za kusaidia hali hiyo kutokana na janga la corona na hivyo kusababisha kuwepo na sera za kubana matumizi, amesema Gourinchas.
IMF imepunguza kiwango cha makadirio yake ya ukuaji wa uchumi kutoka 4.4% hadi 3.6 5, huku benki kuu ya dunia ikipunguza kutoka 4.1 % hadi 2%.
Bei za mafuta na bidhaa zinaendelea kuongezeka na kusababisha kupungua kwa kiwango cha uzalishaji huku mfumuko wa bei ukiongezeka, msemaji wa White house Jen Psaki anailaumu Moscow.
“Tangu mwanzo, tumesema haya kwamba uvamizi wa rais wa Russia Vladmir Putin nchini Ukraine utaendelea kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia, utaathiri soko la mafuta na sekta nyingine,” amesema.
Mhadhiri wa uchumi katika chuo kikuu cha George Washington hapa Marekani Prof Diana Furchtgott-Roth, anasema kwamba ukuaji mdogo wa uchumi wa China kutokana na amri za kila mara za kusitisha shughuli za kawaida kutokana na janga la virusi vya Corona pia umechangia.
“China imeweka amri za watu kutotoka nje kwa shughuli za kawaida. Hiyo ina maana kwamba watengenezaji wa vitu muhimu wanaotumia teknolojia kutoka nje ya nchi kama Korea kusini hawapati vitu hivyo kutengeneza vitu muhimu ndani ya China. La pili, kuna mizigo mingi iliyokwama bandarini kutokana na amri za watu kubaki majumbani katika miji kama vile Hong Kong na Shanghai,” ameeleza mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha George Washington.
Hilo litakuwa ni lengo muhimu kwa wakuu wa benki kuu za nchi tofauti duniani wanaokutana katika mkutano wa IMF na benki kuu unaofanyika Washington DC, kukabiliana nalo ili kupunguza mfumuko wa gharama ya maisha na kuepusha dunia kuingia katika matatizo mabaya zaidi ya kiuchumi, kwa kuongeza kiwango cha riba.